Tangaza Biashara yako hapa

Saturday, December 24, 2011

Tshisekedi ajiapisha nyumbani kwake DRC

Kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi amejiapisha mwenyewe nyumbani kwake baada ya kuzuiliwa kutoka nyumbani.
Majeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yameziba njia ya kwenda kwenye uwanja wa michezo ambapo kiongozi mkuu wa upinzani alipanga kujiapisha.
Etienne Tshisekedi amekataa kukubaliana na ushindi rasmi wa Rais Joseph Kabila katika uchaguzi uliofanyika Novemba.
Mwandishi wa BBC Thomas Hubert kwenye mji mkuu, Kinshasa alisema kuna ulinizi wa hali ya juu katika uwanja huo.
Lakini msemaji wa Bw Tshisekedi aliiambia BBC kiongozi huyo wa UDPS bado alikuwa na nia ya kujiapisha.
Rais Kabila aliapishwa kwa muhula wa pili siku ya Jumanne kufuatia kutangazwa kuwa mshindi rasmi baada ya kupata asilimia 49 ya kura zote, ukilinganisha na asilimia 32 za Bw Thisekedi.
Waangalizi kutoka nchi za kimagharibi walitoa shutuma kwamba matokeo hayo ya urais yana mapungufu makubwa, lakini tume ya uchaguzi- inayoungwa mkono na umoja wa Afrika- ulisifia uchaguzi huo kuwa na mafanikio.
Shirika la kutetea haki za binadamu lenye makao yake makuu Marekani Human Rights Watch (HRW) limesema polisi wameua takriban watu 24 tangu uchaguzi huo wenye utata kufanyika.


Etienne Tshisekedi

Siku ya Alhamisi, chama cha Union for Democracy and Social Progress cha Bw Tshisekedi kilituma kwa kile kinachoonekana mialiko rasmi kwenye karatasi zenye anuani rasmi, ikitaka waandishi wa habari na wanadiplomasia kuhudhuria sehrehe za kuapishwa kwake siku ya Ijumaa asubuhi.
Lakini mwandishi wetu alisema alikataliwa kuingia kwenye uwanja huo wa michezo na barabara zote zinazozunguka makazi ya Bw Tshisekedi kwenye mji mkuu zimewekewa vizuizi.
Kulingana na shirika la habari la AFP, polisi wametumia mabomu ya kutoa machozi kusambaza wafuasi wa upinzani waliozunguka nyumba hiyo.
Polisi na jeshi wote wamesambazwa kwenye uwanja wa Martyr mjini Kinshasa, ambapo ni ngome ya upinzani, mwandishi wetu alisema.
Vifaru, mabomba ya maji na askari wenye bunduki na maguruneti nao walionekana.
Mwandishi wetu alisema, polisi wamewakamata watu kadhaa wakati walipojaribu kuingia unwajani humo.
Wanadiplomasia wamekuwa wakisistiza kuwepo na majadiliano juu ya uchaguzi huo, lakini watu kadhaa wamefariki dunia katika ghasia zilizotokea mjini Kinsahsa na maeneo mengine yaliyo ngome za upinzani tangu uchaguzi uanze.
Uchaguzi wa Novemba ulikuwa wa pili DRC tangu vita vya 1998-2003, vilivyosababisha vifo vya watu takriban milioni nne.
Siku ya Alhamis, tume ya uchaguzi ilisimamisha uhesabuji wa kura za wabunge, ikisema inahitaji msaada wa kimataifa kukamilisha hatua hiyo kufuatia madai ya udanganyifu.
Bw Tshisekedi aliongoza kampeni za kuwepo demokrasia chini ya aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Mobutu Sese Seko lakini huu ni uchaguzi wake wa kwanza kugombea.
Aligomea uchaguzi wa mwanzo wa mwaka 2006, ulioandaliwa chini ya usimamizi wa umoja wa mataifa, baada ya kudai uchaguzi ulifanyiwa hila.
Uchaguzi huo uligubikwa na wiki kadhaa za mapigano mitaani na wafuasi wa mgombea aliyeshindwa, Jean-Pierre Bemba.
Kwa sasa anakabiliwa na kesi katika mahakama ya kimataifa ya ICC kwa madai ya makosa ya uhalifu wa kivita katika nchi jirani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Friday, December 23, 2011

AC Milan na Man City kumjadili Tevez

Makamu Rais wa klabu ya AC Milan Adriano Galliani atafanya mazungumzo na klabu ya Manchester City siku ya Alhamisi juu ya uwezekano wa uhamisho wa Carlos Tevez.
Carlos Tevez akiwa na binti yake Ezeiza nchini Argentina
Carlos Tevez akiwa na binti yake Ezeiza nchini Argentina
Galliani ataelekea Manchester kuzungumzia uhamisho na maafisa wa Manchester City.
Inaaminika Manchester City itamruhusu mshambuliaji huyo kujiunga na Milan kwa mkopo mwezi wa Januari iwapo klabu hiyo ya Italia itatoa uhakikisho wa kumchukua kwa mkataba wa kudumu msimu ujao wa usajili.
Awali Milan ilikuwa tayari kutoa kitita cha euro milioni 23 sawa na paundi milioni 19.3 kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji huyo, lakini vinara hao wa Ligi Kuu ya Kandanda ya England walikataa.
Mabingwa hao wa ligi ya Serie A kwa wiki kadha wamekuwa wakimfuata Tevez, kikwazo kikiwa makubaliano ya uhamisho wake.
Galliani amethibitisha mkutano na Manchester City ulipangwa tangu siku ya Jumatatu.
Amesema: "Siku ya Alhamisi tuna mihadi na Manchester City kuhusiana na suala la Tevez, lakini huenda isiwe kikao kitakachotoa uamuzi wa mwisho wa mazungumzo yetu.
"Hatuendi kumchukua hapo hapo, tutawaeleza tupo tayari kumchukua kwa mkopo na baadae kumnunua mwezi wa Juni.
"Mchezaji mwenyewe anataka kujiunga nasi na si PSG - [Paris St Germain] na tuna matumaini Manchester City wataafiki."
Kwa sasa Tevez yupo kwao Argentina akiwa amekwenda huko bila ya ruhusa ya mwajiri wake tangu mwezi wa Novemba.
Pia amekuwa akihusishwa na klabu ya Paris St Germain, lakini mkurugenzi wa kandanda wa klabu hiyo ya Ufaransa Leonardo amesema hawatapambana na AC Milan iwapo wataweza kukamilisha taratibu za uhamisho wake.
Leonardo, mchezaji na meneja wa zamani wa Milan ameliambia gazeti moja la Ufaransa la La Repubblica: "Sitawaibia Milan Tevez".

Man United yalalamikia mgao wa tikiti

Manchester United imelalamika kwa Chama cha Kandanda cha England -FA- kuhusiana na mgao wao wa tikiti kwa mpambano wa Kombe la FA mzunguko wa tatu mwezi Januari dhidi ya Manchester City.
Uwanja wa Etihad mjini Manchester
Uwanja wa Etihad wa timu ya  Manchester City
Chini ya taratibu za FA, Manchester United wana haki ya kupata mgao wa asilimia 15 ya uwezo wa viti 47,805 katika uwanja wa Etihad, ambao ni sawa na tikiti 7,100.
Hata hivyo, Manchester City imetoa tikiti 5,500, ikiwa ni asilimia 11 tu, hii ni kutokana na sababu za usalama uwanjani.
Manchester United ina mgawanyo maalum kutoka kwa FA, kutokana na uwezo wa uwanja wake wa Old Trafford wenye viti 76,000, kutoa asilimia 11 ya tikiti kwa timu ngeni, sawa na tikiti 8,500.
Mashateni hao Wekundu wanadai wapatiwe mgao wao kamili kwa ajili ya pambano hilo, litakaloanza saa saba mchana siku ya Jumapili tarehe 8 mwezi wa Januari.
Manchester City, ambao kwa sasa wanashikilia usukani wa Ligi Kuu ya England, watawakaribisha mahasimu wao hao wakubwa Manchester United katika mtanange huo wa Kombe la FA kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1955.
Timu hizo zilikutana katika hatua ya nusu fainali mwaka jana kwenye Kombe la FA uwanja wa Wembley, ambapo Manchester City waliibuka washindi kwa bao 1-0 , baadae wakailaza Stoke katika fainali na kufanikiwa kushinda mashindano makubwa kwa mara ya kwanza kwa kipindi cha miaka 35.
Manchester City iliwaadhibu Man United walipokutana mara ya mwisho kwa mabao 6-1 katika mchezo wa Ligi Kuu ya England kwenye uwanja wa Old Trafford.

John Terry kufikishwa mahakamani

Nahodha wa Timu ya Taifa ya England John Terry anakabiliwa na mtihani wa kufunguliwa mashtaka ya uhalifu kwa kutumia lugha ya ubaguzi wa rangi dhidi ya mchezaji mwenzake Anton Ferdinand wakati wa mchuano wa Ligi kuu.
Nahodha wa Chelsea
John Terry
Inasemekana kua John Terry alitumia lugha ya ubaguzi wakati wa pambano kati ya klabu ya Chelsea na Queens Park Rangers iliyomalizika kwa ushindiwa QPR mnamo tarehe 23 Oktoba.
Huduma inayohusika na mashtaka(CPS) inasema kua Bw Terry anakabiliwa na mashtaka ya ukiukaji wa sheria ya ubaguzi wa rangi hadharani.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31 ameapa kujitahidi kwa ala kulla hali kukabili madai hayo.
Polisi imemhoji mchezaji huyo wa Chelsea kwa tahadhari tangu mwezi Novemba na faili kuhusu suala hilo kutumwa kwenye huduma za mashtaka mwanzoni mwa mwezi huu wa Disemba.
Alison Saunders, Mwanasheria mkuu wa jiji la London, amesema kua ameishauri Polisi ya mji mkuu kumfungulia mashtaka John Terry kwa matamshi yake ya kuchukiza kinyume cha sheria inayohusu ubaguzi wa rangi.
Chama cha mpira, FA kiliahirisha upelelezi wake kikisubiri uwamuzi wa Huduma ya mashtaka ukamilike.
Kutokana na hatua ya hivi sasa Bw.Terry anatarajiwa kufika mbele ya Koti ya Mahakama ya London ya magharibi ifikapo tarehe 1 Febuari.
Akipatikana hatia atatozwa hadi pauni za Uingereza 2,500.
Uwamuzi juu ya kesi ya John Terry unatokea siku moja baada ya mshambuliaji wa klabu ya Liverpool Luis Suarez kuhukumiwa kifungo cha kukosa mechi nane za Ligi kwa kumtukana beki wa klabu ya Manchester United - Patrice Evra.

Yaya Toure Mchezaji bora

Mcheza kiungo wa klabu ya Manchester City na pia Timu ya Taifa ya Ivory Coast,Yaya Toure amechaguliwa kua mchezaji bora wa soka na Shirikisho la soka ya Afrika(CAF)
Toure
Yaya Toure
Mchezaji huyo mashuhuri alipitia mchujo wa ushindani na Seydou Keita kutoka Mali anayechezea klabu ya Barcelona na Andre Ayew wa Ghana pia klabu ya Olympique Marseille.
Toure, mwenye umri wa miaka 28, alichaguliwa na Makocha wa Timu za Mataifa ya Afrika kutoka nchi wanachama wa CAF.
Mwenyewe Yaya Toure alisema baada ya kutangazwa kua mchezaji bora kua, ''Hii ndio zawadi kubwa ambayo ningeweza kuipokea katika maisha ya uchezaji wangu soka.''
Inakumbukwa kua Yaya Toure ndiye aliyefunga bao pekee la klabu yake ilipoibwaga Stoke City katika fainali ya Kombe la FA mnamo mwezi Mei.
Toure aliyekua amebubujika kwa furaha alisema kua anajivunia tuzo hio na ni siku kuu kwake, na kuongezea kua ana imani hilo litaipa Timu yake ya Ivory Coast msukumo wakati wakiazimia kushinda Kombe la Mataifa ya Afrika hapo mwakani.
Ushindi wa Toure ulihitimisha furaha ya nchi yake ya Ivory Coast ambayo ilikua tayari inasherehekea mshindi wa zawadi ya Refa bora wa CAF iliyomwendea Noumandiez Doue.
Mchezaji chipukizi aliyejitokeza ni mchezaji mchanga anayechezea klabu ya Tottenham, Souleyman Coulibaly aliyeshinda zawadi ya mchezaji bora mdogo mwenye kipaji. Oussama Darragi wa klabu ya Esperance akachaguliwa ,chezaji bora anayecheza soka yake barani Afrika kama mchezaji bora wa mwaka.
Kocha wa mwaka alikua Harouna Doula aliyeiongoza Timu ya Taifa ya Niger hadi kufuzu kwa fainali za fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika huku Botswana nayo ilitajwa kama mojapo ya Timu zilizofuzu kwa mara ya kwanza kabisa.
Timu ya Wanawake ya Cameroon ilitajwa kua Timu bora ya soka ya wanawake huku Mwanamke bora miongoni mwa wachezaji waliotia fora akiwa Perpetual Nkwoche wa Nigeria.