Kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi amejiapisha mwenyewe nyumbani kwake baada ya kuzuiliwa kutoka nyumbani.
Majeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yameziba njia ya kwenda kwenye uwanja wa michezo ambapo kiongozi mkuu wa upinzani alipanga kujiapisha. Etienne Tshisekedi amekataa kukubaliana na ushindi rasmi wa Rais Joseph Kabila katika uchaguzi uliofanyika Novemba.
Mwandishi wa BBC Thomas Hubert kwenye mji mkuu, Kinshasa alisema kuna ulinizi wa hali ya juu katika uwanja huo.
Lakini msemaji wa Bw Tshisekedi aliiambia BBC kiongozi huyo wa UDPS bado alikuwa na nia ya kujiapisha.
Rais Kabila aliapishwa kwa muhula wa pili siku ya Jumanne kufuatia kutangazwa kuwa mshindi rasmi baada ya kupata asilimia 49 ya kura zote, ukilinganisha na asilimia 32 za Bw Thisekedi.
Waangalizi kutoka nchi za kimagharibi walitoa shutuma kwamba matokeo hayo ya urais yana mapungufu makubwa, lakini tume ya uchaguzi- inayoungwa mkono na umoja wa Afrika- ulisifia uchaguzi huo kuwa na mafanikio.
Shirika la kutetea haki za binadamu lenye makao yake makuu Marekani Human Rights Watch (HRW) limesema polisi wameua takriban watu 24 tangu uchaguzi huo wenye utata kufanyika.
Lakini mwandishi wetu alisema alikataliwa kuingia kwenye uwanja huo wa michezo na barabara zote zinazozunguka makazi ya Bw Tshisekedi kwenye mji mkuu zimewekewa vizuizi.
Kulingana na shirika la habari la AFP, polisi wametumia mabomu ya kutoa machozi kusambaza wafuasi wa upinzani waliozunguka nyumba hiyo.
Polisi na jeshi wote wamesambazwa kwenye uwanja wa Martyr mjini Kinshasa, ambapo ni ngome ya upinzani, mwandishi wetu alisema.
Vifaru, mabomba ya maji na askari wenye bunduki na maguruneti nao walionekana.
Mwandishi wetu alisema, polisi wamewakamata watu kadhaa wakati walipojaribu kuingia unwajani humo.
Wanadiplomasia wamekuwa wakisistiza kuwepo na majadiliano juu ya uchaguzi huo, lakini watu kadhaa wamefariki dunia katika ghasia zilizotokea mjini Kinsahsa na maeneo mengine yaliyo ngome za upinzani tangu uchaguzi uanze.
Uchaguzi wa Novemba ulikuwa wa pili DRC tangu vita vya 1998-2003, vilivyosababisha vifo vya watu takriban milioni nne.
Siku ya Alhamis, tume ya uchaguzi ilisimamisha uhesabuji wa kura za wabunge, ikisema inahitaji msaada wa kimataifa kukamilisha hatua hiyo kufuatia madai ya udanganyifu.
Bw Tshisekedi aliongoza kampeni za kuwepo demokrasia chini ya aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo Mobutu Sese Seko lakini huu ni uchaguzi wake wa kwanza kugombea.
Aligomea uchaguzi wa mwanzo wa mwaka 2006, ulioandaliwa chini ya usimamizi wa umoja wa mataifa, baada ya kudai uchaguzi ulifanyiwa hila.
Uchaguzi huo uligubikwa na wiki kadhaa za mapigano mitaani na wafuasi wa mgombea aliyeshindwa, Jean-Pierre Bemba.
Kwa sasa anakabiliwa na kesi katika mahakama ya kimataifa ya ICC kwa madai ya makosa ya uhalifu wa kivita katika nchi jirani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati.
No comments:
Post a Comment