Makamu Rais wa klabu ya AC Milan Adriano Galliani atafanya mazungumzo na klabu ya Manchester City siku ya Alhamisi juu ya uwezekano wa uhamisho wa Carlos Tevez.
Galliani ataelekea Manchester kuzungumzia uhamisho na maafisa wa Manchester City.
Inaaminika Manchester City itamruhusu mshambuliaji huyo kujiunga na Milan kwa mkopo mwezi wa Januari iwapo klabu hiyo ya Italia itatoa uhakikisho wa kumchukua kwa mkataba wa kudumu msimu ujao wa usajili.
Awali Milan ilikuwa tayari kutoa kitita cha euro milioni 23 sawa na paundi milioni 19.3 kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji huyo, lakini vinara hao wa Ligi Kuu ya Kandanda ya England walikataa.
Mabingwa hao wa ligi ya Serie A kwa wiki kadha wamekuwa wakimfuata Tevez, kikwazo kikiwa makubaliano ya uhamisho wake.
Galliani amethibitisha mkutano na Manchester City ulipangwa tangu siku ya Jumatatu.
Amesema: "Siku ya Alhamisi tuna mihadi na Manchester City kuhusiana na suala la Tevez, lakini huenda isiwe kikao kitakachotoa uamuzi wa mwisho wa mazungumzo yetu.
"Hatuendi kumchukua hapo hapo, tutawaeleza tupo tayari kumchukua kwa mkopo na baadae kumnunua mwezi wa Juni.
"Mchezaji mwenyewe anataka kujiunga nasi na si PSG - [Paris St Germain] na tuna matumaini Manchester City wataafiki."
Kwa sasa Tevez yupo kwao Argentina akiwa amekwenda huko bila ya ruhusa ya mwajiri wake tangu mwezi wa Novemba.
Pia amekuwa akihusishwa na klabu ya Paris St Germain, lakini mkurugenzi wa kandanda wa klabu hiyo ya Ufaransa Leonardo amesema hawatapambana na AC Milan iwapo wataweza kukamilisha taratibu za uhamisho wake.
Leonardo, mchezaji na meneja wa zamani wa Milan ameliambia gazeti moja la Ufaransa la La Repubblica: "Sitawaibia Milan Tevez".
No comments:
Post a Comment