Tangaza Biashara yako hapa

Monday, November 28, 2011

Ulemavu Sio Laana Wala Mkosi

Mwanasheria Josephati Tonner akisisitiza jambo wakati wa uchangiaji wa ujenzi wa kituo cha kulelea watoto walemavu Lamadi wilayani Magu Mkoani Mwanza

Wananchi wameaswa kuwachukua watoto wenye ulemavu kama sehemu ya familia na kuacha tabia ya kuwatenga na kuwaona wao kuwa ni laana au mkosi katika familia zao kwani kila mtu ni mlemavu ila tunatofautiana katika viwango vya ulemavu.

Hayo yamesemwa na mwanasheria mwenye ulemavu wa ngozi Bw. Josephati Tonner katika uchangiaji wa ujenzi wa kituo cha kulelea watoto wenye ulemavu mwishoni mwa wiki katika kijiji cha Lamadi wlayani Magu na kuongeza kuwa kila mtu ni mlemavu na wengi ulemavu tulionao hauonekani kwa macho ya kawaida.

Amesema jamii inatakiwa kuelimishwa kwa wingi ili kupunguza unyanyapaa uliopo hivi sasa kwani elimu ndio msingi wa mabadiliko yoyote yanayotokea kote duniani na ulemavu sio laana kwani hayo ni mawazo mgando ambayo jamii inatakiwa kupewa elimu ya kutosha ili kuondokana na mawazo hayo.

Keflene John Mtoto Mwenye Ulemavu Wa Miguu Anaesoma Darasa La Kwanza Katika Shule Ya Msingi Lutubiga Lamadi Wilayani Magu Ni Mmoja Watoto Watakaokuwa Wakiudumiwa Na Kituo Hicho.


Akisoma risala kwa mgeni rasmi afisa mauhusiano wa kituo hicho kilichopewa jina la The Mary Mother Of God Of Perpertual Help Center chenye usajili No. MDC/CBO/397 amesema kituo hicho kinategeme kuwa shule ya awali, shule ya msingi, secondary na chuo cha ufundi ili kuwapa fursa watoto wenye ulemavu kupata elimu.

 
Akijibu risala mgeni rasmi mwanasheria Josephati Tonner amesema watoto walemavu wakiwezeshwa na kupewa fulsa ya kutosha ulemavu walionao hauwezi kuwa kikwazo katika maisha yao na alijitolea mfano yeye mwenyewe kuwa kama Baba yake asingemsomesha kwakuwa ni albino basi leo maisha yake yangekuwa mabaya sana lakini fulsa aliyopewa leo hii ni msaada kiwi kwake na watu wengine wengi wasio na idadi.

BwanaTonner avenges kuwa kituo hicho hakitakiwi kutegemea misaada kutoka nje ila wakazi wa Lamadi ndio wanaotakiwa kuwa wafadhili wakubwa wa kituo hicho kwani wanaopatiwa msaada ni watoto wao wenyewe hivyo wanatakiwa kujitoa kwa ajili yao

Nae mwanzilishi wa kituo hicho Sister Maria Helen amesema kituo hicho kwasasa kimepata majengo ya muda ya kukodi wakati wakendelea na mchakato wa ujenzi na pia amewashukuru wananchi wa Lamadi na maeneo ya jirani kwa michango yao ya hali na mali katika kufanikishwa upatikanaji wa vitu mbalimbali katika uanzishwaji wa ujenzi wa kituo hicho ambacho kwa nafasi kubwa kitakuwa msaada kwa wakazi wa eneo hilo na maeneo ya jirani.

Bw. Josephati Tonner Akiwa na Mwandishi wa Habari Asia Hamad Mwenye Blauzi Nyekundu Na Sister Maria Helen Aliyevaa Vitenge Na Wageni Wengine Wakati Wa Kutembelea Majengo Yaliyokodishwa Kwa Muda Kwaajili Ya Kituo Hicho

Haya Ndo Majengo Yaliyokodishwa Kwaajili Ya Kuanza Kwa kituo Cha The Mary Mother Of God Of Perpertual Help Center


Saturday, November 26, 2011

Serikali yatakiwa kuzikabili bidhaa za China

TANZANIA inahitajika kuwa na sera kwa ajili ya kusimamia viwanda vinavyozalisha nguo na ambavyo vinatumia pamba inayolimwa hapa nchini, ili kuleta ushindani kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka China ambazo zimekuwa zikiingizwa nchini kwa kiasi kikubwa.

Mkurugenzi wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu Mzumbe iliyopo jijini Dar es Salaam, Profesa Andrew Mbwambo alisema hayo wakati akibadilishana mawazo na wasomi wenzake, viongozi wa serikali na watu wenye uzoefu katika uzalishaji katika sekta ya nguo ili kuweza kukamilisha utafiti anaoufanya na ambao unafanywa na wataalamu wa nchi saba za Afrika Mashairiki na Kusini mwa Afrika.

“Utafiti huu upo katika hatua ya awali kukamilika na unafanywa na nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika ambao unatarajia kuona ni jinsi gani nchi hizi zinajiadaa kuikabili nchi ya China inayokuja kwa kasi sana katika bidhaa za nguo ambazo zipo katika kila kona ya nchi hizi Tanzania ikiwa mojawapo,” alisema Profesa Mbwambo.

Alisema nchi zinazofanya utafiti huo ni pamoja na Kenya, Afrika Kusini, Ethopia, Lethoto, Madascar, Swaziland na Tanzania na lengo siyo kuwa kama China bali kuwa na mikakati ya kujiandaa ili kukabili na kusaidia kukuza uchumi na kuongeza ajira.

Alisema katika utafiti wake huo kwa upande wa Tanzania anatafuta kujua kwa nini viwanda hivyo baada ya kubinafsishwa vinakufa na vingine vimebaki kama vilivyo ili kufahamu tatizo na baadaye kuweza kuishauri serikali hatua za kuchukuliwa.

“Sasa hivi tunaendelea na utafiti, tumeona tuwashirikishe wazalishaji wenyewe kutoka viwandani, watunga sera na wasomi na baada ya kupata sababu ya kuelewa kuhusu tatizo hili tutaandika mapendekezo ya sera ili tuweze kuwa na sera nzuri katika eneo hili,” alisema Profesa Mbwambo.

Alisema nchi ikiwa na sera nzuri ya eneo hili la viwanda vya kuzalisha nguo itatoa fursa ya kutonyanyaswa na bidhaa za kutoka China na hiyo itatoa fursa tena kwa wakulima wa Pamba kupata soko la uhakika na nchi kufaidika zaidi.

Profesa Mbwambo alisema nchi ikiwa na viwanda vingi na kuweza kuuza nguo nzuri za Pamba, mablanketi mazuri na  viatu kama inavyofanya kampuni ya Sun Flag Textile ya Arusha ambayo inauza nguo Marekani, Ulaya, India na Afrika ya kati na Mashariki taifa litapiga hatua kwa kasi kubwa kimaendeleo.

Alisema kukiwepo na Sera maalumu ya kuongoza viwanda vya nguo kama ilivyo kuwa huko nyuma nchi iliweza kuwa na viwanda vingi kwa kuwa baada ya kubinafsisha viwanda wawekezaji hao wengine waliamua kuuza kama chuma chakavu sasa lazima kuwe na sera ya kuongoza eneo hilo.

“Wataalamu wanasema kunatofauti ya soko huru na soko huria, soko huru hata ukienda Marekani kuna taratibu ambazo zinatakiwa kufuatwa kwamba lazima iwe na ubora na ukikosea moja huwezi kufanya biashara lakini soko huria ni kuingiza kila takataka”alisema Profesa Mbwambo.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ukanda wa Uwekezaji (EPZA), Dk Adelhelm Meru akifungua washa hiyo alisema anashukuru utafiti huo ambao unaendelea kufanyika kwa kuibua masuala muhimu ambayo yatakuwa ni msaada wa nchi kuweza kuwa na sera nzuri katika eneo la sekta ya viwanda vya nguo ili kukabili bidhaa za nguo zinazotoka nje ya nchi.

“Utafiti huu unahusisha watalaamu mbalimbali kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, Chuo Kikuu cha Nairobi na Vyuo vingine vya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kwa lengo la kuona maendeleo ya zao la Pamba na sekta nzima ya viwanda vya  nguo kuona tunajifunza nini ukizingatia China inapiga kasi kubwa na bidhaa zao zimetapakaa katika nchi hizi,” alisema Dk Meru.

Alisema ukweli ni kwamba huko nyuma Tanzania ilikuwa ikifanya vizuri sana kulikuwa na viwanda vya Mutex, Mwatex, Urafiki na Sunguratex lakini kwa kufikia miaka ya 1990 vilikufa kutokana na uchumi wa dunia kutetereka.

Alisema kwa sasa Serikali inafanya juhudi za makusudi kuhakikisha inafanya vizuri na uzoefu unaonyesha kuwa sekta ya viwanda ndiyo muhimu sana kwa uchumi wa nchi na utoaji wa ajira kwa wananchi.

Alisema Tanzania ni nchi inayozalisha Pamba kwa wingi laikini kwa bahati mbaya inauzwa nje ya nchi ikiwa ghafi ndiyo maana Serikali inahamasisha uwekezaji ili pamba hiyo iweze kutumika katika viwanda vya hapa nchini badala ya kuuzwa ikiwa ghafi.

Benki Ya Kiislam Yazinduliwa

WAFANYABIASHARA wanaofuata misingi ya dini ya Kiislamu wameanzisha benki mpya ya Kiislamu  (Amana Benki L.T.D) itakayoendeshwa kwa kufuata sheria na taratibu za dini hiyo  nchini.

Benki hiyo imezinduliwa jijini Dar es Salaam jana baada ya  kupata leseni ya muda kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT)Februari 4 mwaka huu na kusajiriwa  ikiwa na mtaji wa Sh100 bilioni ulioidhinishwa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi  ya Amana Benki, Haroon Pirmohamed aliwaambia waandishi wa habari katika hafla ya uzinduzi kuwa benki hiyo itawawezesha  wafanyabiashara na makundi mbalimbali ya dini hiyo kufanya shughuli zao za kifedha bila kuathiri misingi ya imani yao.

"Hili ni jambo la imani, hivyo huduma hii itawasaidia wafanyabiashara na watu wa makundi mbalimbali kuendesha biashara zao za kibenki bila kuathiri imani yao,”alisema  Pirmohamed.

Alifafanua kuwa pamoja na huduma zitakazotolewa na benki hiyo kufuata misingi ya dini ya Kiislamu, zitawahusu pia watu wa makundi yote wakiwamo wa dini nyingine wanaoamini katika mfumo wa kibenki unaofuata sharia.

Alitaja moja ya misingi iliyomo katika mfumo wa sharia za Kiisilamu  kuwa ni kuendesha benki isiyotoza riba.

Parimohamed alizitaja huduma zitakazotolewa na Benki hiyo kuwa ni akaunti za akiba, akaunti ya watoto, wanawake, Hijja, hundi, biashara na akiba kwa ajili ya akiba pia na nyumba za ibada zilizosajiliwa.
CHASEMA KUJIVUA GAMBA,VITA YA UFISADI VIKO PALEPALE
Neville Meena na Habel Chidawali, Dodoma
Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama akitoa taarifa kwa waandishi wa habari, jana, juu ya maazimio yaliyotolewa kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho uliofanyika kwa siku mbili mkoani Dodoma.Kulia ni Makamu Mwenyekiti Bara Pius Msekwa Picha na Edwin Mjwahuzi

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kwa mara ya kwanza kimekiri hadharani kuwa mbio za Urais wa mwaka 2015 ni miongoni mwa mambo yanayokitikisa na sasa kinachukua hatua za kuwadhibiti makada wake wenye nia hiyo ili harakati zake zisikiathiri.Kadhalika, CCM kimesema dhana ya kujivua gamba kiliyoiasisi iko palepale na kwamba utekelezaji wake unaanza mara moja kwa kuwachukulia hatua wanachama wake wote wanaotuhumiwa kwa rushwa na ufisadi.

Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama aliwaambia waandishi wa habari jana Mjini Dodoma kuwa si vibaya makada wa chama hicho kuanza kufikiria urais wa 2015 lakini tatizo ni njia ambazo zinatumika katika harakati hizo.

“Sisi hatuna shida na watu hao kwa kuwa ni haki yao, lakini lazima watumie njia sahihi ambazo hazitaleta shida kwa chama na tumeona iko haja ya kutengeneza mfumo mzuri wa kupata mgombea urais ambaye hatatokana na fedha isipokuwa akubalike kwa uwezo wake wa kujenga hoja, itikadi yake na kile anachokiamini,” alisema Mukama.

Mukama alikiri kuwa mbali na mbio za urais 2015, pia CCM kinateswa na siasa za makundi ambayo yamekuwa yakitumika kushambuliana, kinyume cha maadili yake.

Alisema CCM kinachukua hatua za kukabiliana na makundi ambayo misingi yake hujengwa katika chaguzi za ndani ya chama, na kwamba watahakikisha hilo halitokei wakati wa uchaguzi wake unaotarajiwa kufanyika mwakani.

“Kwa maneno ambayo tuliyatumia tulisema, hii kansa ya kupangana safu inaweka mtu ambaye hata sifa wala hana habari kabisa na matatizo ya wananchi, wala haumii lakini anapanga safu… lazima tuondokane na kansa hii ili tupate viongozi wanaojali na wanaohangaika na maisha ya wavuja jasho wa nchi hii,” alisema.

Kujivua gamba

Kuhusu suala la kujivua gamba, akimaanisha kuchukua hatua dhidi ya watuhumiwa wa makosa mbalimbali ukiwemo ufisadi na rushwa, Katibu Mkuu huyo alisema kati ya maazimio 26 yaliyotolewa na NEC Aprili mwaka huu, Azimio namba 27 “linahitaji kutekelezwa haraka iwezekanavyo.”

“Dhana hiyo ya kukipatia chama chetu sura mpya ndiyo iliyopewa jina la kujivua gamba na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa imekwishatengeneza mpango wa utekelezaji wa uamuzi huo,’’ alisema Mukama.

Alisema katika kikao chake kilichomalizika juzi, NEC imeamua kuwa viongozi wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi ndani ya chama walipaswa kujipima na kujitafakari wenyewe na ikibidi wachukue hatua jambo ambalo halijatekelezwa hadi sasa.

Alisema Azimio hilo liliwalenga viongozi katika ngazi zote za chama kuanzia taifa hadi tawi na kilichokusudiwa ni kujenga utamaduni wa kusimamia maadili ya viongozi na wanachama wake.

“Takriban miezi saba baada ya Azimio hilo kupitishwa, bado hatujapata mwitikio wa kuridhisha kutoka kwa viongozi wa ngazi yoyote wa chama chetu ambao ni walengwa wa azimio,’’ alisema na kuongeza:

“Bila shaka sasa wakati umefika wa chama kutekeleza ile sehemu ya pili ya azimio husika kwa kuwawajibisha wahusika, lakini utekelezaji wake hauna budi ufanyike kwa kufuata utaratibu uliowekwa ndani na kanuni za CCM za uongozi na maadili.’’

Msingi wa mpango wa kujivua gamba umejengwa katika azimio la NEC linalosema: “Viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi watafakari, wajipime na kuchukua hatua wao wenyewe kwa maslahi ya chama, wasipofanya hivyo, chama kiwawajibishe bila kuchelewa.”

Lakini tangu kupitishwa kwa mpango huo Aprili mwaka huu, ni kada mmoja tu, Rostam Aziz aliyechukua hatua za kujiuzulu Ubunge wa Jimbo la Igunga na Ujumbe wa NEC huku wengine wakiwa kimya.

Mukama alisema sehemu ya pili ya azimio hilo inayosema: “Wasipofanya hivyo chama kiwawajibishe bila kuchelewa,” ndiyo msingi wa NEC kurejesha suala hilo kwa Kamati Kuu na kwamba sasa litafanyika katika ngazi zote.
Alisema NEC imeziagiza kamati za siasa kupitia kamati za ulinzi usalama na maadili kwa ngazi zote kuanza mara moja, mchakato wa kutekeleza azimio hilo kwa mujibu wa kanuni na taratibu za chama.

Alisema NEC iliagiza kazi hiyo kufanyika haraka bila kuchelewa na baada ya kukamilika kwa kazi hiyo, taarifa zipelekwe kwenye vikao vya kikatiba vya uamuzi kwa hatua za utekelezaji.

Alisema chama hicho kitahakikisha kwamba ajenda hiyo haitekwi na makundi yanayokinzana na kwamba lengo zima ni kuhakikisha kwamba CCM kinaongeza uwezo wa kusimamia mambo yake na Serikali zake zote.

“Lazima kifike mahali (CCM), kiwe na uwezo wa kuzisimamia na kuhakikisha kwamba Serikali zinatekeleza matakwa ya wananchi na siyo vinginevyo, ndiyo maana watu wanajiunga na vyama kwani huwa wanatarajia watapata utetezi,” alisema Mukama.

Kuhusu vurugu na migomo ya vyuo vikuu CCM kiliagiza Serikali kuchukua hatua za haraka kukabiliana na hali hiyo na kuitaka kusimamia sheria inayokataza uendeshaji wa shughuli za kisiasa katika taasisi za elimu nchini. Kimetaka wanafunzi na watumishi wabanwe ili waendeshe shughuli hizo nje ya taasisi husika.

Kuhusu suala la Nishati nchini, Mukama alisema NEC imeiagiza Serikali kuhakikisha kuwa inapunguza bei za mafuta na hasa ya taa ambayo yanatumiwa na wananchi wengi wenye kipato cha chini.

Juzi, Mawaziri Wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, waliwashambulia kwa maneno makali wajumbe wawili wa Sekretarieti ya CCM kwamba wamekuwa wakikivuruga chama na kusababisha mgawanyiko uliopo kwa jinsi ambavyo wamekuwa wakisimamia mpango wa kujivua gamba.

Lowassa aliyejiuzulu Uwaziri Mkuu, kutokana na kashfa ya Richmond ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzungumzia suala hilo wakati wa mjadala wa hali ya siasa, pale alipowataja Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Tanzania Bara, John Chiligati kwamba wamekuwa wakitukana watu ovyo kwa fedha wanazopewa na CCM.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Lowassa alitumia zaidi ya dakika saba kumshambulia Nape kwamba amekuwa akifanya mambo nje ya utaratibu na kwamba mwenendo huo umekuwa ukikibomoa chama badala ya kukijenga.

Sumaye alisimama na kuhoji sababu za chama hicho kunyamazia ukiukwaji wa taratibu ambao umekuwa ukifanywa na watendaji hao.

Lowassa, Sumaye wabwatuka CCM

WALIA KUCHAFULIWA NA MAKADA WENZAO,NEC YARIDHIA GAMBA KUREJESHWA CC
 Neville Meena na Habel Chidawali, Dodoma
MAWAZIRI Wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye, jana walishambulia kwa maneno makali wajumbe wawili wa Sekretarieti ya CCM kwamba wamekuwa wakikivuruga chama na kusababisha mgawanyiko uliopo.Lowassa aliyejiuzulu Uwaziri Mkuu, kutokana na kashfa ya Richmond ndiye aliyekuwa wa kwanza kuzungumzia suala hilo wakati wa mjadala wa hali ya siasa, katika kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kilichomazika jana mjini Dodoma.

Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho zinasema Lowassa alianza kubwaga moyo wake baada ya NEC kuridhia ombi la Kamati Kuu ya chama hicho (CC) kwamba suala la mageuzi ndani ya CCM maarufu kama kujivua gamba lirejeshwe katika kamati hiyo ili lifanyiwe kazi kwa taratibu za kawaida za kinidhamu baada ya wahusika kukataa kuachia nafasi zao.

“Mwenyekiti kwanza napongeza uamuzi huu wa kurejesha jambo hili katika taratibu za kawaida, lakini napenda kufahamu kwa miezi saba nimetukanwa nikiitwa fisadi, watu wamezunguka nchi nzima kwa fedha za chama wakinitukana, hivi hatukujua kwamba kuna kamati hizo za maadili,”Lowassa alinukuliwa akihoji.

Lowassa alinukuliwa akiwataja Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye na Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho, Tanzania Bara, John Chiligati kwamba wamekuwa wakitukana watu ovyo kwa fedha wanazopewa na CCM.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, Lowassa alitumia dakika saba kumshambulia Nape kwamba amekuwa akifanya mambo nje ya utaratibu na kwamba mwenendo huo umekuwa ukikibomoa chama badala ya kukijenga.

Baada ya maneno ya Lowassa, Waziri Mkuu mstaafu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Sumaye alisimama na kuhoji sababu za chama hicho kunyamazia ukiukwaji wa taratibu ambao umekuwa ukifanywa na watendaji hao.

“Mwenyekiti huyu bwana (Lowassa) amesema kwamba amechafuliwa kwa miezi saba, sasa kama leo tunasema kwamba tunarudi kwenye utaratibu wa kamati za maadili, hao waliomchafua watafanywaje?”Sumaye alinukuliwa akihoji.
Hata hivyo, taarifa za ndani ya kikao hicho zilimnukuu Kikwete akisema kwamba viongozi hao watakuchukuliwa hatua za kinidhamu kama watakuwa wamefanya hivyo.
Kutokana na hali hiyo, Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete aliwasihi wajumbe kuachana na suala hilo na badala yake kuchangia maeneo mengine ya taarifa hiyo ya hali ya siasa iliyowasilishwa na Katibu wa Siasa na Mambo ya Nje ya CCM, January Makamba.

Kikwete alinukuliwa akihitimisha hoja hiyo kwa kusema kwamba: “Jamani hapa tunajenga chama, watu wanasubiri kusikia tukimaliza kikao chetu kwa ugomvi, naomba tumalize kwa amani na twendeni tukajenge chama chetu”.

Richmond yatajwa
Vyanzo vyetu vilimnukuu Lowassa akizungumzia suala la Kampuni tata ya kufua umeme ya Richmond kwamba yeye aliamua kuvunja mkataba baina ya kampuni hiyo, lakini Rais KIkwete alimwambia subiri baada ya kuwa amepata ushauri wa Makatibu Wakuu.

Lowassa ambaye ni Mbunge wa Monduli (CCM), alinukuliwa akisema: “Mwenyekiti utakumbuka kwamba mimi nilishaamua kuvunja mkataba wa Richmond mapema, lakini baada ya kukupigia simu ukiwa katika safari nje ya nchi ulisema tusubiri kwani ulikuwa umepata ushauri wa makatibu wakuu wa wizara, sasa leo hii ninahukumiwa nakuitwa fisadi kwanini?”.

“Nilijiuzulu kuwajibika kwa ajili ya kuilinda Serikali yangu na kwa heshima ya chama changu, sasa kwanini leo nahukumiwa kwa jambo hili, tena natukanwa na wana CCM wenzangu na siyo wapinzani nchi nzima kwamba mimi eti fisadi?,”alinukuliwa akihoji Lowassa.

Kadhalika kada huyo wa CCM alinukuliwa akimkumbusha Rais Kikwete kwamba: “Mwenyekiti nikukumbushe mwaka 1997 kule Zanzibar, kina Mzee Daudi Mwakawago walikuja na mafaili yakiwa na tuhuma dhidi ya mtizamo hasi wa jamii dhidi yako, kwa hiyo wakati ule kama si busara za kina Mzee Mkapa (Benjamin) leo usingekuwa hapo ulipo”.

Lowassa alisema kama alivyozungumza na Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa walipokutana jijini Dar es Salaam, tatizo kubwa analolifahamu la vita ya sasa ni urais wa 2015.

“Mwenyekiti nikukumbushe jambo jingine, kule Zanzibar mwaka 1997 walipoleta tuhuma za mtizamo wa umma dhidi yako, ulisema kwamba kuwa Rais ni mipango ya Mungu,”alinukuliwa Lowassa katika maelezo yake ndani ya NEC

Alisema kwa kuzingatia mazingira hayo, hii leo si sahihi hata yeye (Lowassa) kuhukumiwa kwa kuzingatia kile kinachodaiwa kuwa ni mtizamo wa umma dhidi yake unaompa sura ya ufisadi, jambo ambalo alidai kwamba siyo la kweli.
Baada ya Lowassa na Sumaye kuongoa, kada maarufu wa chama hicho, Kingunge Ngombale Mwiru alisimama akitaka kuongelea dhana ya gamba ndipo Mkapa alipomshtua Kikwete kwamba hoja hiyo ifikie mwisho.
Baadhi ya wajumbe waliiambia Mwananchi kwamba wakati Lowassa akiongea Mkapa alionekana kufurahi.

Kujivua gamba
Kufuatia uamuzi huo wa NEC hivi sasa mpango wa kujivua gamba ulioasisiwa na chama hicho, Aprili mwaka huu unarejeshwa CC ambapo watuhumiwa wote wa makosa mbalimbali watafikishwa mbele ya Kamati za maadili na kuchukuliwa hatua kwa taratibu za chama hicho.

Mpango wa kujivua gamba ulilenga kuwashinikiza watuhumiwa wa ufisadi kuachia nafasi zao za uongozi ndani ya chama hicho na sasa unarejeshwa Kamati Kuu (CC) ili ichukue hatua zaidi kwa wale waliogoma kujiuzulu.

Hatua hiyo inatokana na kuwapo ukimya ambao unaashiria kutokuwapo viongozi na makada ambao wako tayari kujiuzulu nyadhifa zao kwa hiari yao kama ilivyotarajiwa.

Tangu kupitishwa kwa mpango huo maarufu kwa jina la kujivua gamba katika kikao cha NEC kilichopita cha Aprili mwaka huu, ni kada mmoja tu, Rostam Aziz aliyechukua hatua za kujiuzulu ubunge wa Jimbo la Igunga na ujumbe wa NEC, lakini wengine wamekuwa kimya hadi sasa.

Katika kikao cha Aprili NEC hiyo ya CCM ilipitisha maazimio 26, lakini kubwa ni lile lililokuwa likihimiza vita dhidi ya ufisadi kuendelea na kutoa mwito kwa watu wanaotajwa na jamii kuhusika na ufisadi ambao wako ndani ya chama kujitathmini kisha kuchukua hatua za kuachia madaraka waliyonayo.

Sehemu ya mwisho ya azimio hilo inasomeka: “Wasipoachia madaraka chama kiwachukulie hatua mara moja”.

Mmoja wa wajumbe wa CC ambaye ameomba jina lake kuhifadhiwa alisema: “Tunawaomba NEC waturuhusu jambo hili tulifanyie kazi sisi (CC) na litafanyiwa kazi kupitia taratibu za kawaida za chama kwa kuzingatia kanuni na taratibu za maadili za chama hicho”.

Nec yawakaanga kina Jairo
Katika hatua nyingine, NEC imeunga mkono hatua zilizopendekezwa na Bunge dhidi ya watumishi wa umma waliotajwa katika ripoti ya Kamati Teule ya Bunge, iliyoanika uozo wa matumizi mabaya ya fedha za Umma ndani ya Wizara ya Nishati na Madini.

Kamati hiyo katika ripoti yake iliyowasilishwa mwishoni mwa Mkutano wa Tano wa Bunge uliomalizika wiki iliyopita mjini Dodoma, iliwataja Katibu Mkuu, Wizara ya Nishati na Madini (aliyesimamishwa), David Jairo na Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo kwamba wanastahili kuchukuliwa hatua.

Wengine ni Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh, huku wabunge wakipendekeza pia kuondolewa madarakani kwa Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Adam Malima.

Ugugaji Wa Kuku Wa Kienyeji Unaweza Kukukwamua Kiuchumi





Watu wengi wamekuwa wakifikiria kuhusu namna ya kujikwamua kutoka kwenye umasikini.Leo hii nitawaelezea kuhusu biashara ya kufuga kuku wa kienyeji ambavyo inaweza kukukwamua kutoka kwenye umasikini. Lengo kuu ni kuwawezesha watu kutengeneza ajira kwao binafsi na watu wengine.
Takwimu za uzalishaji (kutaga, kuangua na kukuza kuku)


Utafiti uliofanywa na Dr. John Bishop kwa msaada wa shirika la kitaifa la utafiti wa kilimo nchini Equador na Chuo kikuu cha Florida nchini Marekani, umeonyesha kuwa ; Kama kuku akitunzwa vizuri kutokana na mbinu bora za ufugaji, anaweza Kuongeza uwezo wa kutaga mayai kutoka mayai 10 hadi mayai 12 kwa mwezi. Kwa mfano ukiwa na kuku 12 na jogoo 1 waliolishwa kilo 1 ya nafaka kila siku unaweza kuuza dazani 10 za mayai kila mwezi ambayo ni sawa na mayai 4 kila siku.
Jee unapenda kutajirika kwa kufuga na kuuza kuku?

Angalia mchanganuo wa mahesabu mapato yako yatakuwa kama ifuatavyo, Kwa kipindi cha miaka 2. K wa mtaji wa Sh. 500,000/= kama una eneo la eka 1 na mabanda ya kutosha kiasi cha kuku 10,000. Ukianza kwa kufuga kuku 25 ( kuku 20 na jogoo 5) ambao utawanunua kwa Sh. 250,000.00. Hao kuku 20 wakianza kutaga vifaranga 10 kila mmoja wataangua vifaranga 200 watunze vizuri katika vifaranga hao tuchukulie majike yanaweza kuwa 150 ambao ndani ya miezi 6 au zaidi nao wataanza kutaga. Kipindi hicho utakuwa na kuku (200+ 25 =225.) Baada ya hiyo miezi 6 kuku watakaotaga ni 170 kila mmoja akipata vifaranga 10 mpaka mwisho wa mwaka utakuwa na kuku (1700+20+55=1775) ukiuza kuku 1,000 kwa bei ya Tshs. 10,000 utapata Tshs. 10,000,000/=. Mwaka wa 2 majike 775 yakiangua vifaranga 10 kila mmoja utakuwa na kuku 7,550 mwisho wa mwaka ukiuza kuku 3,000 kwa bei ya Tshs. 10,000 utapata Tshs. 30,000,000/= Hesabu hizi ni kwa makadirio ya chini sana kwani kama nilivyoelezea hapo juu kuku mmoja kama atatunzwa vizuri anaweza kuataga mayai kati ya 10 hadi 12 kwa mwezi.

.Kuku wa kienyeji wamekuwa wakifugwa kwa wingi vijijini kwa malengo ya kupata nyama na mayai kwa ajili ya familia husika na kwa ajili ya kupata pesa za kujikimu. Kuku na mayai ya kienyeji yana faida kubwa kiafya kutofautisha na kuku wakisasa ambao hukuzwa kwa kemikali. Idadiya kuku Tanzania inakadiriwa kuwa na jumla ya kuku Milioni 34 wanaofugwa na takribani 60.5% ya kaya zinazojishughulisha na kilimo. Hata hivyo uzalishaji wake umebaki kuwa duni kutokana na changamoto za wafugaji zifuatazo; Utunzaji duni , Udhibiti mdogo wa magonjwa, lishe duni, makazi duni, Uzaliano wa karibu, Teknolojia duni, Kukosekana kwa mtazamo/mwamko wa kibiashara.
Faida ya kufuga kuku wa kienyeji.

Ufugaji wa kuku wa kienyeji una manufaa mengi kwa mfano; Kuku hutumia eneo dogo kuliko wanyama wengine wa kufugwa, pia hutumia chakula kidogo hivyo ufugaji unaweza kuendeshwa bila kutumia mtaji mkubwa.

Kuku wanaweza kupewa mabaki ya chakula pamoja na vyakula vya kujitafutia kama vile wadudu,mbegu na majani. Kazi za usimamizi wa kuku zinaweza kufanywa na mama na watoto.

Kuku na mayai humpatia mfugaji chakula bora na kumuongezea mapato. Pia mfugaji ni kama mtu aliyewekeza fedha zake benki au kwenye kitegauchumi kingine ambapo kuku huweza kuongezeka kutokana na kuku kutaga na kuangua vifaranga kama faida inavoongezeka benki na kwenye vitegauchumi vingine.

Mfugaji ni sawa na mtu aliyeweka akiba benki kwani akipata shida anaweza kuuza kuku na kulipa ada, mahari matibabu ya hospitali pamoja na shida zingine.

Kuku wa kienyeji anasaidia kusafisha mazingira kwa kula wadudu na kuongeza rutuba kwa mbolea inayotokana na kinyesi cha kuku ambacho hakina kemikali.

Mbolea hii ni nzuri sana na kama inazalishwa kwa wingi inaweza kuwa chanzo kingine cha mapato kwa mfugaji wa kuku. Kuna mjasiriamali ninayemjua anafuga kuku wengi anazo tani nyingi za mbolea hii na anauza mbolea ya mavi ya kuku kwa Sh. 600 kwa kiloba cha kilo 50. Kuku wa kienyeji ana uwezo mkubwa wa kuhimili magonjwa, hutaga mayai na kutunza vifaranga badala ya kutumia mashine.

Kuku wa kienyeji anaweza kuishi nchi yoyote duniani bila kuathiriwa na hali ya hewa.
Aina za magonjwa ya kuku na jinsi ya kukinga magonjwa.
Wapatie chanjo kuku wako kwa afya bora.

Wapatie kinga mara kwamara kila baada ya miezi 3. Magonjwa yafuatayo ndiyo huwa yanawashambulia kuku.
New castle

Dalili za ugonjwa huu ni kuku kushindwa kupumua, kukohoa na kutokwa na mate,kuwa na kinyesi cha rangi ya kijani, ugonjwa huu hauna dawa. Chanjo hutolewa machoni kwa njia ya matone.
Minyoo.

Dalili za mionyoo ni kuku kukosa hamu ya kula uzalishaji wa mayai kupungua. Ukiona dalili hizo waone wataalamu wa mifugo upate dawa.
Wadudu.

Utitiri husumbua kuku, kwa kuwasababisha kukosa usingizi,ngozi kuharibika,huathiri uzalishaji wa mayai. Ukiona dalili hizi wasiliana na wataalamu wa mifugo upate dawa.
Magonjwa ya mapafu.

Huathiri sehemu za kupitishia hewa na kuwa na sauti ya kukoroma. Hali hii hupunguza uzalishaji wa mayai na uzito wa kuku kupungua.

Ukiona dalili hizi wasiliana na wataalamu wa mifugo upate dawa.

Mambo mengine unayopaswa kuyajua kama mfugaji wa kuku
Inapokuja katika ufugaji wa kuku wa kienyeji ,mbinu inayotumiwa kijijini ile kuku huachwa azurure katika boma bila uchungaji ama na uchungaji mdogo.Kuna matatizo mengi ambayo kuku hukutana nayo.

Kuku halishwi vyema kwani hula masalio ya.chakula na mabaki mengine wanayoyapata. Vifaranga wadogo huachwa washindanie chakula na kuku wakubwa na huwa nyama rahisi kwa wanyama wanaowinda na kula nyama na husambaza magonjwa.

Kuku hawapati maji ya kutosha na hawana mahali pa kujisetiri dhidi ya upepo na mvua ama kuwaweka salama dhidi ya wanyama wanaowinda na kula nyama bila kusahau wezi.

kuku hutaga mayai ardhini na yanaweza kuharibiwa kwa urahisi na kuliwa na wanyama wengine. Sio kawaida kuku kupewa chanjo na matibabu dhidi ya magonjwa na vimelea.

Matokeo ni kuku wengi huwa wagonjwa na hukua pole pole,hutaga mayai machache na nyama kidogo.

Ili kuhakikisha mapato mazuri kutoka kwa kuku wako,fanya yafuatayo:
Kuwapatia kuku mgao mzuri wa vyakula tofauti na maji safi.Kutemeana na kipindi cha mwaka,wataweza kujitafutia chakula kwa kukwaruza ardhi katika boma.

Wapatie chakula cha ziada ili kuku waongeze uzani na kuku watage mayai mengi zaidi.

Walishe vifaranga na chakula kilicho na protini kama mchwa ili wakue kwa haraka na wawe na afya.

Wajengee kuku mahali penye giza na patulivu ambapo wanaweza kutaga mayai yao.

Kuku huhitaji kujisikia wakiwa salama kutoka kwa wanyama wanaowinda na kula nyama na wapita njia.

Kama kuku watasumbuliwa mara kwa mara watakuwa wakiviacha viota vyao na hii huathiri uanguaji wa mayai.

Ikiwa nia yako ni utoaji wa mayai,ni vizuri kufuga kuku wa kike pekee.

Jogoo mmoja anaweza kufugwa aangalie wanyama wanaowinda na kula nyama na kuwahudumia kuku.

Wakati jogoo wa ziada wanapofikia umri wa kuuzwa,wanafaa kuuzwa,kuchinjwa ama kutolewa kama zawadi kuzuia jogoo kula chakula ambacho ni adimu na kupigana na kuwataabisha kuku.

Ukubwa wa kundi unafaa kuafikiana na ukubwa wa nyumba au banda ,kiasi cha chakula unachoweza kununua na raslimali za chakula katika maeneo yanayokuzunguka.

Usinunue kuku kutoka katika vyanzo ambavyo havijathibitiwa haswa vipindi milipuko ya magonjwa ni kawaida kwa sababu wanaweza kusambaza magonjwa kwa wengine.

Toa chanjo mara kwa mara kulingana na ushauri wa watoaji chanjo na madaktari wa wanyama wa nyumbani.


 Vifaranga wachanga wanapaswa kuchanjwa dhidi ya magonjwa ya kawaida ya kuambukizana wakifika umri wa wiki 2-3.

Ikiwa kuku watataabika kutoka kwa ugonjwa sugu unapaswa:
1. Kuita daktari wa wanyama
2. Kumwtenga kutoka kwa wengine
3.Kuku anafaa kuuliwa mara moja kwa kutegemea jinsi ugonjwa ulivyo mzito na
anafaa kuchomwa ama kuzikwa katika kina kirefu ili kuzuia mbwa na wanyama wengine kuwachimba na kusambaza ugonjwa.
Angalia ni kuku wagani wana dalili za kutaka kuangua mara moja kwa mwezi na uwapatie matunzo ya ziada.

Karoti Ni Dawa Tosha


Kwa ujumla wake, karoti ni mboga yenye kiasi kingi cha Vitamini A. Mbali ya vitamini hiyo, karoti ina virutubisho vingine muhimu vyenye uwezo wa kuzuia magonjwa hatari, kama vile saratani, moyo na mengine mengi na kumbuka kwamba; ‘kinga ni bora kuliko tiba’.

Sifa pekee na kubwa kuhusu karoti inayojulikana na watu wengi, ni uwezo wake wa kuimarisha nuru ya macho na uwezo wa kuona, hususan wakati wa usiku. Katika makala ya leo nitakufahamisha faida nyingine za mboga hii rahisi, inayopatikana kwa wingi, mijini na vijijini. Ukiielewa vizuri, itaokoa maisha yako.


VIRUTUBISHO VYA KAROTI
Kwa mujibu wa tafiti kadhaa zilizofanywa, imethibitika kuwa karoti ina kiwango kikubwa cha virutubisho jamii ya ‘carotenoids’ ambavyo husaidia kuupa mwili uwezo wake wa asili wa kupambana na maradhi yanayojitokeza mwilini.

Katika utafiti huo, imeelezwa kuwa ulaji wa karoti, hata kwa kiasi cha karoti moja tu kwa siku, kinampunguzia mlaji uwezekano wa kupatwa na ugonjwa wa saratani ya matiti kwa asilimia 20.


Aidha, imeainishwa zaidi kuwa, mlaji wa karoti moja kwa siku, atakuwa pia anajiepusha na kupatwa na saratani za aina nyingine kwa asilimia 50. Saratani hizo zimetajwa kuwa ni saratani ya kibofu cha mkojo, kizazi, utumbo, mapafu na saratani ya koo.

Katika utafiti wa hivi karibuni wa Taasisi ya Saratani ya Taifa nchini Marekani (National Cancer Institute), imebainika kuwa wagonjwa wengi waliogundulika na saratani ya mapafu, katika milo yao walikuwa hawatumii karoti wala vyakula vingine vyenye virutubisho jamii ya ‘carotenoids’.

KAROTI NA UGONJWA WA KISUKARI
Kama tujuavyo, ugonjwa wa kisukari ni maradhi yanayowasumbua watu wengi duniani na hauna tiba. Magonjwa kama kisukari, huweza kumpata mtu kutokana na mpangilio mbaya wa vyakula anavyokula kila siku na staili ya maisha anayoishi kwa ujumla.

Mtu anaweza kujiepusha na magonjwa mengi hatari, kama kisukari, kwa kuzingatia ulaji usahihi. Kutokana na kiwango cha virutubisho mbalimbali vilivyomo kwenye karoti, mgonjwa wa kisukari anaweza kupata ahueni kwa kufanya karoti kuwa sehemu ya mlo wake wa kila siku.

Watafiti wamegundua kwamba virubisho vilivyomo kwenye karoti, vina uwezo mkubwa wa kurekebisha kiwango cha sukari mwilini, hivyo kutoa kinga au kumpa mgonjwa nafuu kubwa.

KAROTI NA MAPAFU
Kama unaishi au unafanya kazi katika mazingira yenye moshi au wewe ni mvutaji wa sigara, ulaji wa vyakula vyenye vitamin A kwa wingi kama karoti, humuepusha mvutaji na uwezekano wa kupatwa na saratani ya mapafu. Ulaji wa vyakula aina hii kwa mvuta sigara, si wa hiyari kama anataka kujiepusha na saratani ya mapafu.

JINSI YA KUCHAGUA NA KUHIFADHI KAROTI
Kwa kawaida, karoti huwa ni mzizi ulionyooka wenye rangi za kung’aa. Zipo karoti za rangi tofauti lakini karoti bora ni ile tuliyoizoea yenye rangi ya chungwa na kwa mujibu wa utafiti, karoti yenye rangi iliyoiva sana ndiyo yenye virubisho vingi zaidi.

Karoti inaweza kudumu kwa muda mrefu ikihifadhiwa vizuri. Hifadhi karoti yako kwenye jokofu ikiwa kwenye mfuko wa plastiki ambao hauruhusu kupitisha hewa nyingine, ikihifadhiwa vyema, karoti inaweza kukaa hadi wiki mbili bila kuharibika.

Aidha, wakati wa kuhifadhi karoti yako katika jokofu, usichanganye na matunda mengine kama vile ‘peasi’, nyanya, ‘epo’ na matunda mengine ya jamii hiyo. Inaelezwa kuwa kwa matunda hayo kukaa pamoja, kunaweza kuifanya karoti kuwa chungu.

Kabla ya kuhifadhi karoti kwenye jokofu, hakikisha umekata majani yake ya juu na mizizi yake ya chini, ili kuzuia karoti kuchipua licha ya kuwa kwenye jokofu.

JINSI YA KUANDAA NA KUILA KAROTI
Osha vizuri karoti yako kwa kutumia kifaa maalum cha kusugulia pamoja na maji safi. Wakati wa kuosha karoti, ni vizuri ukitumia maji ya kutiririka na siyo yaliyotuama. Osha karoti kwenye maji ya bomba au kwa kumimina na chombo, usioshee ndani ya chombo kuepuka kuondoka na vijidudu.

Sigara huharibu DNA mwilini na kuongeza hatari ya kupata kensa!


Kemikali za sumu zilizoko katika tumbaku ya sigara huharibu DNA za mwili wa binadamu dakika chache tu baada ya mtu kuanza kuvuta sigara. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa hivi karibuni, kemikali hizo zinazoitwa Polycylic Aromatic Hydrocarbons (PAHs) husababisha DNA ziharibike na kuongeza uwezekano wa mtu kupata kensa. 

Katika uchunguzi huo watalamu walichukua kemikali hizo katika miili ya wavuta sigara na kuzifanyia uchunguzi, ambapo waligundua kuwa, kemikali za PHA hubadilika haraka mwilini na kuwa sumu ambayo huharibu DNA baada ya kupita dakika 15 hadi 30 tangu kuingia tumbaku katika mwili wa binadamu.

Sumu hiyo hubadilisha seli mwilini au kufanya mutation, kitendo ambacho huweza kusababisha kensa. Wataalamu hao wanasema, kitendo hicho hufanyika kwa haraka sana kama vile inavyoingizwa mada ya sumu kwenye damu kwa sindano.

Habari hii ni tahadhari kwa watu wanaotaka kuanza kuvuta sigara, kwani takwimu zinatuonyesha kwamba, watu 3,000 hufariki dunia kila siku umwenguni kutokana na kensa ya mapafu, maradhi ambayo husababishwa kwa asilimia 90 na uvutaji sigara.

Madhara ya kuvuta sigara kwa muda mrefu yanajulikana na wengi, ambayo ni pamoja na magonjwa ya moyo na kensa mbalimbali, lakini wataalamu wanatuasa ya kuwa, madhara ya sigara huanza pale tu mtu anapoanza kupiga pafu ya kwanza na kuingiza moshi wa sigara mwilini. Hivyo bado hujachelewa na unaweza kuacha sigara hii leo! 
Angalia Jinsi Mapafu Pafu Lilivyobadilika Na Kuwa Jeusi Kwasababu Ya Sigara

Kuwaanzisha watoto chakula kigumu miezi 6 mapema kunawasaidia


Maneno haya si yangu, lakini nakumbuka kwa uzoefu wangu siku zote nilikuwa nikipingana na waalimu darasani na mahospitalini kuhusu muda wa kuanzishwa chakula kigumu watoto wanaonyonya au 'weaning'!.

Siku zote walimu wangu chuo kikuu walikuwa wakisema kuwa watoto wachanga wanaonyesha waanzishwe vyakula vingine wanapokuwa na miezi minne, lakini mie nikipinga na kusisitiza kwamba muda huo utumike kwa watoto wenye asili ya kizungu au weupe, lakini kwa uzoefu wangu, watoto wetu wa Kiafrika tunawaanzisha chakula kigumu wanapokuwa na miezi minne, kwani ifikapo muda huo maziwa ya mama zao huwa hayawatoshi tena! Pia hata wadau wa Kona ya Afya pale waliponiomba ushauri niliwashauri hivyo.

Hoja yangu hiyo imethibitishwa hivi karibuni na timu moja ya Uingereza ambayo ilifanya utafiti na kuchapisha utafiti huo katika Makala ya Tiba ya Uingereza. Wanatimu hiyo wamesema, kutegemea tu maziwa ya mama pekee kwa watoto hadi miezi sita sio vizuri na hayatoshi. Wamesema maziwa ya mama yanaweza kuwa na faida iwapo watoto wataanzishwa vyakula vinginevyo mapema hasa baada ya miezi minne.

Huko nyuma wataalamu walishauri kuwa mtoto apewe maziwa ya mama pekee hadi miezi sita lakini hivi sasa wamebadilisha msimamo huo na wanashauri mtoto aanze kupewa chakula kingine akiwa na miezi minne huku akiendelea kunyonyeshwa. Miaka 10 iliyopita Shirika la Afya Duniani lilitoa muongozo kwamba, watoto wachanga wanyonyeshwe maziwa ya mama pekee hadi miezi 6!
Utafiti mwingine umeonyesha kuwa, watoto wachanga wanaocheleweshwa kuanzishwa chakula kigumu hupatwa na upungufu wa damu au anemia kuliko wale wanaoanzishwa vyakula vingine wakiwa na miezi minne hadi 6.

Hata hivyo wazazi na walezi wametakiwa kuzingatia aina ya vyakula wanavyowapa watoto wao wachanga pale wanapofikia muda wa kuanza kula, kwani baadhi ya vyakula huwasababishia allergies na pia kufanya wakose choo.

Jeshi Misri 'lamteua Waziri Mkuu' mpya

Kamal Ganzouri

Watawala wa kijeshi nchini Misri wamemteua waziri mkuu wa zamani Kamal Ganzouri aweze kuunda serikali mpya, shirika la habari la serikali limesema
.
Baraza la mawaziri la kiraia lilokuwa limeteuliwa na jeshi lilijiuzulu mapema wiki hii wakati maandamano yalipoanza mjini Cairo na miji mingine.
Baraza la kijeshi limesema kwa uchaguzi wa wabunge utaanza wiki ijayo kote nchini kama ilivyopangwa.

Makabiliano karibu na medani ya Tahrir yamepungua lakini wanaharakati wanakataka kuwe na maandamanano siku ya Ijumaa.
Idadi kubwa ya waandamanaji wanalala katika medani ya Tahrir wakijiandaa kwa mkutano mkubwa siku ya Ijumaa.

Baraza kuu linalotawala la kijeshi linasimamia mchakato wa mabadiliko hadsi katika utawala wa kiraia kufuatia kupinduliwa kwa Rais Hosni Mubarak mwezi Februari.

Licha ya ahadi za baraza hilo kuharakisha mchakato wa mabadiliko, raia wengi wa Misri wanaogopa kuwa jeshi lina nia ya kuendelea kubaki madarakani.

Bwana Ganzouri aliongoza serikali ya Misri kutoka mwaka 1996 hadi mwaka 1999 chini ya utawala wa Bwana Mubarak.

Gazeti la serikali al-Ahram limesema katika tovuti yake kwamba kimsingi Bwana Ganzouri amekubali kuongoza serikali baada ya kukutana na kiongozi wa baraza la kijeshi Mohamed Hussein Tantawi.

Bwana Ganzouri, ambaye amejitenga na utawala wa Bwana Mubarak, amependekezwa kama mgombea wa urais.

Friday, November 25, 2011

Ijumaa nyengine maandamano mengine

  Waandamanaji mjini Cairo wamekusanyika kwa maandamano mengine wakiwataka viongozi wa kijeshi wa Misri wang'atuke mamlakani.

 Umati mkubwa wa watu umeshiriki katika swala ya Ijumaa katika medani ya Tahrir ambako kumekuwa na waandamanaji kwa kipindi cha wiki moja.

Waandamanaji wanataka uchaguzi wa Jumatatu uahirishwe.
Msururu wa sasa wa maaandamano umesababisha ghasia kubwa kuwahi kutokea tangu kung'olewa mamlakani Hosni Mubarak mwezi Febbruary.Watu zaidi ya 40 wameuawa katika ghasia hizo.

Baraza kuu la kijeshi-SCAF- ndio linalosimamia utaratibu wa kurejesha utawala kwa raia.
Licha ya ahadi za kuachia madaraka na kuharakisha utaratibu huo , baadhi ya waandamanaji wanahofu kuwa huenda viongozi hao wa kijeshi wananuia kung'ang'ania madaraka. Waandamanaji wanataka utawala wa kijeshi kuondoka kabla ya uchaguzi wa wabunge kufanywa.
Majeruhi katika maandamano Misri
Majeruhi katika maandamano Misri
Wakati huohuo raia wengi wa Misri wanataka uchaguzi uendelee kama ulivyopangwa. Kundi moja lenye ushawishi mkubwa nchini humo linalojulikana kama "Muslim Brotherhood" ambalo linatarajiwa kufanya vizuri katika uchaguzi, haliwaungi mkono waandamanaji katika medani ya Tahrir.

Wakati hayo yanaendelea maandamano ya kuunga mkono uchaguzi yanaandaliwa karibu na jengo la wizara ya mashauri ya ndani. 

Huko Washington, Ikulu ya White House imesema madaraka nchini Misriyanapaswa yahamishiwe kwa raia haraka iwezekanavyo.

Taarifa kutoka Ikulu ya White House ilisema "Marekani inaamini kuwa serikali mpya ya Misri inapaswa ipewe mamlaka kamili na thabit haraka iwezekanavyo."

Televisheni ya taifa ilisema kuwa jeshi limemteua aliyekuwa wakati mmoja Waziri Mkuu Kamal Ganzouri kuunda serikali mpya baada ya aliyemtangulia kujiuzulu.

Maelfu ya watu walikusanyika katika medani ya Tahrir kushiriki katika kile waandaaji wanasema ni Ijumaa ya mwisho ya fursa ya kutoa dukuduku lao la kutaka jeshi liachie utawala.

Shirika la AFP limesema kuwa Imamu aliyeongoza swala ya Ijumaa mjini Cairo alitoa wito kwa jeshi kuachia madaraka na kusema kuwa waandamanaji watasalia katika medani hiyo hadi matakwa yao yatakapotimizwa.

Waandamanaji wameushutumu uteuzi wa Bw. Ganzouri ambaye aliongoza serikali ya Misri kutoka mwaka 1996 hadi 1999 chini ya Hosni Mubarak.

Tatizo la kukosa choo watoto wadogo au kuwa na choo kigumu na jinsi ya kulitatua



Tatizo la kukosa choo watoto wadogo au kuwa na choo kigumu na jinsi ya kulitatua
Watoto wadogo hasa wale ambao bado wananyonya na ndio kwanza wamenzishwa vyakula vinginevyo zaidi ya maziwa, mara nyingi hupatwa na choo kigumu au kukosa choo kabisa hali tunayoiita kimombo, constipation. 

Hali hiyo huanza pale mtoto anapoachishwa maziwa ya mama na kuanza kunyweshwa maziwa ya kopo au mengineyo au pia anapoanzishwa kula vyakula vingine zaidi ya maziwa. Mara nyingi watoto wanaonyonya maziwa ya mama huwa hawasumbuliwa na tatizo hilo, bali tatizo hilo huanza kujitokeza pale wanapoanza kulishwa vyakula vingine zaidi ya maziwa ya mama. Pia mama ambaye tayari mwenyewe anasumbuliwa na tatizo la kukosa choo, huenda mwanae pia akasumbuliwa na tatizo hilo.

Mtoto mwenye tatizo la kukosa choo huwa anapata choo wa shida huku akisumbuliwa na tumbo na kupata choo kigumu. Wakati mwingine hulia wakati akipata choo huku akijiminya na kukunja uso. Muone daktari iwapo mtoto ana umri wa chini ya mwezi mmoja na hajapata choo kwa siku 4.

Iwapo mtoto wako mchanga au mdogo ana tatizo la kukosa choo au kupata choo kigumu kwanza wasiliana na daktari au mpeleke hospitalini ili upate ushari wa daktari. Pia unashauriwa kujaribu njia zifuatazo:

1. Jaribu kumpa mtoto wako maji safi na salama kuanzia mililita 60 hadi 120 kwa siku. Punguza au ongeza kiasi hicho kwa kuzingatia jinsi hali ya mwanao inavyokuwa. Ni bora maji ya mtoto yachemshwe na kufunikwa vyema.

2. Iwapo maji hayasaidii, jaribu pia kumpa juisi za matunda. Mpe mtoto wako juisi ya tufaha (apple), pea au prune iliyotengenezwa kwa kutumia maji salama na safi kila siku. Anza kwa mililita 60 hadi 120 kwa siku na punguza au ongeza kiasi hicho kwa kuzingatia jinsi hali ya mwanao inavyokuwa.

3. Jitahidi kumpa mwanao chakula chenye ufumwele au fiber. Iwapo mwanao ameanza kula vyakula vigumu, basi mpe vyakula vyenye ufumwele kuliko vyakula vyenye wanga, kama vile tumia unga wa shayiri au tunda la apple na pea lililopondwa pondwa vyema na kuwa kama uji. Epuka kumpa mtoto cereal ya mchele au uji wa mchele kama anatatizo la kukosa choo au kufunga choo.

4. Jiepushe kumpa mtoto wako vyakula vyenye wanga na sukari na vyakula vinavyotengenezwa kwa unga uliokobolewa.

5. Mpake mwanao mafuta kidogo sehemu inayotoka choo kikubwa ili kurahisisha utokaji wa kinyesi. Usitumia mafuta ya madini (mineral oil) au dawa za kulainisha choo na za kuharishwa katika kutibu tatizo hilo la kukosa choo la mtoto.

6. Kukosa choo watoto wadogo mara chache huwa kunasababishwa na magonjwa kama vile Hirschsprung ugonjwa wa kumee neva katika utumbo, au Cystic Fibrosis. Muone daktari au mpeleke mtoto wako hospitalini kama tatizo hilo la kukosa choo linaendelea hata baada ya kubadilisha aina ya chakula cha mtoto au linaambatana na dalili nyingine kama vile kutapika au mtoto kukosa utulivu na kuhangaika.

7. Kuna baadhi ya watoto wanakosa choo au kuwa na choo kigumu kutokana na kutumia maziwa ya ng’ombe. Iwapo umetumia dawa na umefuata maelekezo ya kuondoa ukosefu wa choo na hukufanikiwa. Katisha kumpa mtoto maziwa ya ng’ombe kwa siku mbili au tatu, baada ya siku hizo iwapo bado hajaacha choo badi endelea kumpa maziwa hayo, na pengine tatizo hilo halisababishwi na maziwa ya ng’ombe.

8. Mwogeshe au mweke mwanao katika beseni la maji ya uvuguvugu na hakikisha maji yanafika hadi kifuani. Mkande mtoto tumbo lake wakati akiwa majini na njia hiyo husaidia kulegeza misuli ya mwili wa mtoto, na kumsaidia kupata chook wa urahisi.

N.B Ukosefu wa choo kwa watu wazima baadhi ya wakati huandamana na magonjwa kama vile Arthritis, Appendicitis, Cataract, saratani, shinikizo la damu, Rheumatism na kadhalika lakini kwa watoto huenda tatizo hilo likawa halisababishwi na maradhi hayo.

Utafiti unaonyesha kuwa hakuna uhusiano wowote kuhusu kukosa choo mtoto na kupewa nyongeza ya chuma au Iron Supplement. Hivyo usimkatishe kumpa mwanao chuma iwapo anakosa choo. Kwani chum ni muhimu sana katika kuzuia upungufu wa damu mwilini kwa mtoto wako mdogo.

Kila siku faida za Folic Acid zazidi kugunduliwa


Katika hali ambayo muda mrefu imekuwa ikifahamika kwamba dawa za folic acid zinazotakiwa kuliwa na mama wajawazito zina faida kemkem kwa watoto wanozaliwa, wataalamu hivi karibuni wameendelea kufahamu umuhimu wake zaidi.

Siku zote kina mama wajawazito wamekuwa wakishauriwa kula folic acid miezi mitatu kabla ya kushika mimba, na pia kwa miezi kadhaa wakati wa ujauzito.

Utafiti wa hivi karibuni umeonyesha kwamba watoto ambao mama zao walikula folic acid kabla na wakati wa ujauzito kwa kiasi kikubwa huwa hawachelewi kuzungumza.

Uchunguzi huo uliofanywa huko Norway kwa kuwashirikisha wanawake 40,000 umebainisha kwamba wale ambao hawakula folic acid kabla na wakati walipokuwa na mimba wana uwezekano mara dufu wa kuzaa watoto wenye matatizo ya kuchelewa kuongea kuliko waliokula. Kwa mujibu wa utafiti huo uliochapisha kwenye Jarida la Marekani la Taasisis ya Tiba (JAMA) kula folic acidi wiki 4 kabla ya ujauzito na kuendelea hadi wiki 8 baada ya kutungwa mimba husaidia kupunguza hatari ya watoto kushindwa kuongea hata wanapofikia miaka mitatu.

Ingawa wataalamu wamekiri hawajui ni namna gani folic acid inazuia watoto kuchelewa kuongea lakini wanasema, kuna uwezekano dawa hizo zikawa zinataathira katika mfumo wa neva na kuzuia tatizo hilo lisitokee.

Folic acid ni miongoni mwa tembe zinazohusiwa sana mama wajawazito kula, kwani inajulikana kuwa zinazuia watoto wachanga kuzaliwa wakiwa na ugonjwa unaoitwa 'neural tube defects' ambao ni matatizo katika sehemu ya chini ya ute wa mgongo ambapo mtoto mchanga huzaliwa huku ubongo wake ukiwa haukukua kabisa. Lakini ingawa hayo yote yanajuliakana shaka yangu ni kuwa je, mama wajawazito katika nchi zetu wanajua hilo au je, wanaelimusha juu ya umuhimu wa kula folic acid? Nadhani ni jukumu langu mie na wewe kuielimisha jamii.

Majaribio ya chanjo ya kwanza ya malaria yaonyesha mafanikio



Majaribio ya chanjo ya ugonjwa wa malaria yameonyesha mafanikio na hivyo kuleta matumaini kuwa huenda gonjwa hilo sugu linalohatarisha maisha ya mamilioni ya watoto barani Afrika likapatiwa chanjo kwa mara ya kwanza duniani. Taarifa kuhusu awamu za mwisho za majaribio ya chanjo hiyo inayotengenezwa na shirika la GlaxoSmithKline zilitangaza Jumanne ya wiki hii na kuonyesha kwamba ina uwezo wa kuulinda mwili dhidi ya malaria kwa watoto wenye umri wa miezi mitano hadi 17.

Andrew Witty Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo la kutengeza dawa la Uingereza ambalo limetengeneza chanjo hiyo amesema kwamba, mafanikio hayo yanaonyesha kuwa hivi karibuni dunia kwa mara ya kwanza itaweza kupata chanjo ya ugonjwa wa Malaria.

Hata hivyo sambamba na kusifu mafanikio hayo Bw. Witty amesisitiza kwamba wanasayansi wanaoshulighulia ugonjwa huo na wataalamu wa masuala ya afya ulimwenguni kote bado wanasisitiza kwamba chanjo hiyo inayojulikana kana RTS,S au Mosquirix bado sio njia ya haraka ya kutokomeza malaria. Licha ya hayo inaelezwa kuwa chanjo hiyo ya aina ya sindano haina athari sana katika kuzuia ugonjwa wa malaria ikilinganishwa na chanjo nyingine kama vile za ugonjwa wa polio na ndui.

Gonjwa la malaria bado ni janga kubwa kwa nchi nyingi duniani hasa za Afrika zilizo chini ya Jangwa la Sahara na kila mwaka hupelekea vifo vya watu wengi kwenye nchi hizo hasa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

Chanjo sio changamoto pekee inayowakabili wataalamu wa masuala ya afya na tiba duniani katika kupambana na malaria bali tiba ya ugonjwa huo pia imekuwa ikibadilika mara kwa mara kutokana na vidudu vya ugonjwa huo kujibadili na kuzishinda nguvu dawa zinazotengeneza za kutibu ugonjwa huo.

Kwa ajili hiyo madaktari na wataalamu wamekuwa wakishauri kutumiwa zaidi tiba ya dawa mseto katika kutibu malaria kuliko dawa moja pekee.

Njia nyingine za kujilinda na malaria ni pamoja na kutumia chandarua, kupiga dawa za kuua mbu na kuyaweka mazingira tuishiyo katika hali ya usafi bila kuwepo vindimbwi vya maji na kuzungukwa na vichaka suala ambalo husababisha mbu wazaane.

Ingawa habari hii ni mafanikio makubwa yanayopaswa kupigiwa makofi na wadau wote wa masuala ya afya na tiba lakini, shaka yangu mie ni kuwa, hata kama chanjo hiyo ikianza kufanya kazi kesho lakini je, watoto wote wa bara Afrika wataweza kupatiwa chanjo hiyo na kuepusha na vifo vya holela vinavyosababishwa na malaria? Au isije ikawa hadithi zile zile za chanjo ya polio na ndui ambazo zimekuwepo kwa miongo mingi lakini mpaka leo bado kuna watoto wa Kiafrika wasiopatiwa chanjo hizo kutokana na sababu mbalimbali.

Maghembe ahimiza zana bora kilimo cha tumbaku


Serikali imewaasa wakulima wa tumbaku duniani kupuuza vitisho na upinzani dhidi ya zao hilo na badala yake walime zao hilo kwa wingi zaidi huku wakifuata kanuni na taratibu za ulimaji wa zao hilo kama zilivyowekwa na serikali zao.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa juzi na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe, wakati akifungua Mkutano wa Asasi ya Kimataifa ya Wakulima wa Tumbaku(ITGA).

Aidha, Waziri Mghembe amewataka wadau wa tumbaku katika nchi zinazoendelea kuchagiza mabadiliko ya wakulima wao ili wafikie viwango vya wale wa nchi tajiri duniani, ikiwemo kuachana na zana za kilimo duni kama vile jembe la mkono ambalo hudumaza kipato cha wakulima.

"Wakati umefika sasa kwa wakulima wetu kubadilika na ili wawafikie wenzao wa nchi tajiri kwa kutumia mikopo ili kubadilisha zana za kilimo, na badala yake watumie jembe la ng’ombe na matrekta. Tutakapofikia hapo huu wastani wa 0.8 hadi hekta moja kwa mkulima tutaachana nao,” alisema katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mohammed Muya.

Profesa Maghembe aliishauri sekta ya tumbaku kuchukua hatua dhidi ya upotevu wa zao hilo wakati wa mavuno, ambapo kwa sasa wakulima hupoteza hadi asilimia 35, huku akisisitiza umuhimu wa sekta kujikita katika uhamasishaji wa ujenzi wa mabanda kukaushia, kufungia na yale ya kuhifadhia zao hilo.

Profesa Maghembe alisema sekta ya tumbaku ndiyo pekee nchini yenye sera maalum utunzaji mazingira kwa upandaji miti, akitoa mfano kwamba tangu msimu wa mwaka 2009/2010 miti zaidi ya milioni 20 imekuwa ikipandwa na wakulima wa zao hilo kila mwaka nchini.

Alizitaja faida za zao hilo ikilinganishwa na mazao mengine mbadala kama vile bei kubwa na imara wakati wote pamoja na soko la uhakika hivyo huchangia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha na uchumi wa watu vijijini.

Msemaji kutoka kampuni ya Universal Leaf ya Marekani ambayo ni kampuni mama ya Kampuni ya Tumbaku Tanzania (TLTC), Barbara Martelini, alisema wakati umefika kwa sekta hiyo kuelimisha umma namna mambo yanavyokwenda katika sekta hiyo ili kupunguza upotoshaji uliopo.

Msemaji mwingine kutoka Kampuni ya British American Tobacco (BAT), alisema kampuni yake iko makini kutunza biyoanuai miongoni mwa wakulima wa tumbaku ambayo hufanya kazi nao, na inao mkakati maalum wa kuwalemisha wakulima hao waendelee kufanya hivyo wakati wote.

Naye Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Tumbaku nchini (TTB), Frank Urio, alisema tumbaku ni zao muhimu kwa maendeleo ya uchumi wan chi kwani mpaka sasa imeajiri zaidi ya familia 130,000 nchini ambao wamejiunga katika vyama saba vya ushirika wa kilimo.
CHANZO: NIPASHE

Chadema wang`aka mkutano wao na Kikwete kuingiliwa

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), wamepinga ushauri wa Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, kukutana na vyama vyote vya siasa badala ya Chadema peke yake.

Wa kwanza kupinga agizo la CC-CCM ni Chadema kupitia Kaimu Katibu Mkuu wake, Victor Kimesera.
Kimesera, ambaye ni Katibu Mtendaji Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chadema, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa wanaopaswa kukutana na Rais Kikwete ni Chadema peke yake.
Hivyo, akasema Chadema hawako tayari kukubali kushirikiana na chama kingine chochote katika hilo kwa sasa.
“Sisi (Chadema) ndio tulioomba kukutana na Rais Kikwete. Hatukuwaombea wengine. Wao (vyama vingine) kama wana haja ya kukutana na Rais Kikwete waombe siku yao,” alisema Kimesera.
Alisema Chadema ilimuomba Rais Kikwete kukutana naye kwa ajili ya kujadili juu ya mchakato wa kupata kKatiba mpya na hawakuiomba CC-CCM suala hilo.
Kutokana na hilo, alisema wanamuachia Rais Kikwete na vyama vingine vya siasa kuamua lini wakutane. “Maamuzi yafanywe na wahusika, siyo na Kamati Kuu (ya CCM),” alisema Kimesera.
KAFULILA NAYE APINGA
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, amesema haoni mantiki ya agizo hilo la CC-CCM.
“Uamuzi wa kwamba, tukutane vyama vyote na Rais sioni mantiki yake badala yake Rais akutane na wanaotaka kukutana naye,” alisema Kafulila.
Aliongeza: “Binafsi sioni sababu na sitegemei lolote kutoka kikao cha namna hiyo na Rais. Sisi hatukutoka bungeni ili tukutane na Rais baadaye.”
Alisema wanaamini CCM, serikali na hata Rais Kikwete mwenyewe hawana dhamira ya kweli katika ajenda ya katiba tangu mwanzo.
“Na hawatakuwa na dhamira hiyo hata baadaye kwa kuwa katiba wanayotaka wananchi ni msumari kwa chama na serikali ya CCM,” alisema Kafulila, ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa NCCR-Mageuzi Taifa.
Alisema ushahidi unaothibitisha kuwa serikali haiko tayari kwa jambo hilo upo wazi.
Kafulila alisema ushahidi wa kwanza umethibitika katika msimamo wa CCM wa tangu mwanzo kwa kukataa kuweka ajenda ya katiba mpya kwenye Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana, licha ya msukumo wa umma kuhusu suala hilo kuwa mkubwa.
Alisema wa pili, umethibitishwa na Mwansheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, na Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani, ambao kabla ya tamko la Rais Kikwete kuridhia mchakato huo, kwa nyakati tofauti walikaririwa wakisema kwamba jambo hilo halina umuhimu wowote kwa sasa na kwamba, hadi leo bado hawajafuta kauli zao.
Ushahidi wa tatu, alisema Aprili, mwaka huu Baraza la Mawaziri, ambalo Mwenyekiti wake ni Rais, lilipitisha muswada mbovu wa sheria ya mabadiliko ya katiba kuliko miswada yote kiasi cha kuamsha hasira za umma, ambao walidiriki kuuchana hadharani na kutaka urejeshwe serikalini.
Alisema ushahidi wa nne umethibitika muswada huo uliporejeshwa serikalini na baadaye kuletwa mpya, ambapo bado serikali na CCM walishinikiza Bunge lijadili na kupitisha kabla ya umma kupata nafasi ya kujadili kama ilivyotakiwa kwa mujibu wa kanuni.
Jumatatu Chadema kilitangaza kuwa kinataka kukutana na Rais Kikwete kuzungumzia suala la katiba, baada ya wabunge wake kususia mjadala wa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011.
Jumanne, Rais Kikwete aliwajibu kwa kuwakubalia na kuagiza kuwa maandalizi ya mkutano huo yaanze.
Katika kutekeleza azma hiyo ya kuonana na Rais, Chadema iliunda timu ya watu saba chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, ambayo imepewa kazi ya kushughulikia suala hilo.
Wengine ni Katibu Mkuu, Dk. Slaa; Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Said Arfi; Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Issa Mohamed; wajumbe wa Kamati Kuu, Profesa Mwesiga Baregu na Profesa Abdallah Safari pamoja na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Hata hivyo, CC ya CCM juzi ilimshauri Rais Kikwete kukutana na vyama vyote vyenye wabunge kwa ajili ya kupanua wigo wa mawazo kuhusu katiba mpya.
Katibu wa Unezi na Itikadi wa CCM, Nape Nnauye, alisema CCM inaamini kuwa njia ya majadiliano waliyoitumia Chadema katika kutafuta haki ni nzuri na fursa hiyo ikitumiwa vizuri, inaweza kuleta maelewano mazuri na faida kwa jamii.

ASKOFU: WABUNGE HAWAJUI KINACHOENDELEA KATIKA MCHAKATO
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Dk. Owdenberg Mdegella, amesema utata unaojitokeza hivi sasa wa wananchi kuonyesha nia ya kuupinga wazi wazi muswada huo, unatokana na baadhi ya watu, wakiwamo wabunge, kutojua kinachoendelea katika mchakato huo.
Alisema wapo wajanja wachache wanaojua kitakachotokea baadaye katika mchakato huo, lakini wengi wao hawajui kinachoendelea na kwamba, wamo katika kundi linalobebwa katika mchakato huo.
Askofu Mdegella alisema hayo jana wakati akihojiwa na Kituo cha Redio Furaha. “Swali kubwa katika marekebisho ya katiba duniani kote ni hili. Nani anachukua usukani wa kuhakikisha anajua kila sentensi, kila koma pamoja na nukta. Huwa serikali inatumia uzembe wetu wa kutokusoma kuingiza baadhi ya mambo, ambayo hayakuwamo. Hii ni hatari kubwa kama hatutakuwa makini,” alionya Askofu huyo.
Aliilaumu Chadema kwa kususia kushiriki mjadala wa muswada huo bungeni, akidai kwamba, kitendo hicho hakikuwa sahihi kwa kuwa kiliwaruhusu wabunge wa CCM kuupitisha kirahisi.
“Mimi nafikiri kitendo kile cha Chadema kutoka bungeni kwa ajili ya kususia muswada wa sheria ya marejeo ya katiba, hakikuwa sahihi kwa sababu kiliwaruhusu wabunge wa CCM kuupitisha muswada huo kirahisi…Kama wangekuwa ndani, nafikiri CCM wasingeupitisha kirahisi namna hiyo na hapo ndipo hoja yao ingeonekana ina nguvu,” alisema.
Kuhusu madaraka ya Rais, Askofu huyo alisema ni vyema yakapimwa upya na kushauri kuwa katika katiba mpya ijayo, Rais asipewe madaraka makubwa, badala yake apewe madaraka yanayoweza kuhojiwa kikatiba.
CHANZO: NIPASHE

Wabongo Wawili Waula Mamtoni


Watanzania wawili kucheza ligi daraja la pili Sweden Wachezaji wawili wa kitanzania, Joseph Kaniki (Golota) na William John wamefanikiwa kujiunga na timu ya ligi daraja la pili KonyaSpor (KIF) nchini Sweden, baada ya kufanikiwa kupita katika majaribio( Trials). Majaribio hayo yalijumuisha wachezaji zaidi ya thelathini ambapo wachezaji watano walichaguliwa kujiunga na klabu hiyo ya ligi daraja la pili KonyaSpor (KIF)

Sunday, November 20, 2011

Kuna uhuru wa vyombo vya habari katika nchi huru kama Tanzania?




  • Japo Tanzania ni nchi yenye uhuru mkubwa wa habari, mimi nadhani uhuru huu hautumiwi vizuri na ubora wa habari tunazoshindiliwa kila siku hauridhishi. Kwa mfano, ni magazeti machache sana yanayoandika habari za kweli na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina, habari zilizojaa ushahidi, data na hoja hakikifu yakinifu. 
  • Magazeti mengi - hata yale yanayojidai kuwa ni dhati pevu - yamejikita katika kuandika habari zilizofanyiwa uchambuzi nusunusu, habari ambazo japo kwa juu zinaonekana kama za kweli, ukisoma kwa uangalifu utakuta kwamba ama lojiki na hata data zilizotumiwa katika kufanyia majumuisho ya habari hizo hazikubaliki. Matokeo yake habari nyingi zinaandikwa kwa kuripuliwa na zinaonekana kuwa kama za udakudaku tu; na zilizojaa mihemko inayotokana na ushabiki wa kisiasa uliokithiri.
  • Kwa vile udaku ndiyo unaopendwa sana na wasomaji, inawezekana pengine magazeti mengi yanafanya hivi ili yaweze kuvutia wasomaji. Mkanganyiko unazidi zaidi kwa sababu wanajamii wengi bado wanaamini kwamba kila kinachotiwa katika maandishi, kusikika kwenye redio au runinga basi ni lazima kiwe cha ukweli. 
  • Matokeo yake tunakuwa na jamii inayoshabikia mambo bila kuyaelewa sawasawa, jamii iliyojikita katika kuamini udaku na inayoweza kuyumbishwa kirahisi. Ndiyo maana ni rahisi sana kumchafulia mtu jina kama ukitaka. Kama una "bifu" na Matondo na akatokea kuwa na nafasi kubwa katika jamii, basi jidamke na kusema kuwa Matondo ni fisadi na akaunti yake aliyoficha Marekani ina mamilioni ya dola. Na kesho yake utakuta habari hii imetapakaa katika kurasa za mbele za magazeti  - hata yale yanayojidai kuwa makini. 

  • Hakuna gazeti ambalo litakaa chini na kujaribu kutafuta ukweli na kuthibitisha chanzo na uhalali wa habari kama hii. Na kwa vile jamii nayo bado inaamini (na hata kutegemea) kwamba kila kitu kinachoandikwa katika magazeti ni cha ukweli basi kuanzia siku hiyo mlengwa wa habari hizi atajulikana kama fisadi, gamba n.k. Na kama hana ujasiri wa kusimama na kujitetea kama alivyofanya Sumaye hapa chini basi jamii daima itamtazama kwa jicho la hatihati. 
  •  

  • Lengo langu hapa siyo kuwatetea mafisadi na nadhani msimamo wangu kuhusu UFISADI na mambo mengine katika jamii unaeleweka kwa wasomaji wa blogu hii. Ninachokisema hapa ni kwamba, kama jamii ni lazima tuwe makini na habari nusunusu tunazolishwa na vyombo vyetu hivi vya habari. Na litakuwa jambo jema kama tutaweza kuzitambua habari za kidaku kama wenzetu hawa na kuzipa uzito wake unaostahili.   

  • Waandishi wa habari, mnalo jukumu kubwa sana katika ukombozi wa jamii yetu na kabisa msijaribu kuliteteresha jukumu hili zito. Kama tulivyoona katika uchaguzi mkuu uliopita, mabadiliko mema yanatokea  katika nchi yetu na nyakati zinabadilika. Isaidieni jamii katika juhudi za kujitafuta kwake. Shirikini vyema katika kuhakikisha kwamba tunakuwa na jamii makinifu na yenye uwezo wa kuhoji ukweli wa mambo na siyo kushabikia udaku kiholela - jamii ambayo ikidanganywa au kupewa habari au ahadi za kidaku, basi iwe na uwezo wa kusimama na kusema hapa mmetudanganya; na mkiendelea kutudanganya basi tutawanyang'anya madaraka tuliyowapa!