Tangaza Biashara yako hapa

Friday, November 25, 2011

Ijumaa nyengine maandamano mengine

  Waandamanaji mjini Cairo wamekusanyika kwa maandamano mengine wakiwataka viongozi wa kijeshi wa Misri wang'atuke mamlakani.

 Umati mkubwa wa watu umeshiriki katika swala ya Ijumaa katika medani ya Tahrir ambako kumekuwa na waandamanaji kwa kipindi cha wiki moja.

Waandamanaji wanataka uchaguzi wa Jumatatu uahirishwe.
Msururu wa sasa wa maaandamano umesababisha ghasia kubwa kuwahi kutokea tangu kung'olewa mamlakani Hosni Mubarak mwezi Febbruary.Watu zaidi ya 40 wameuawa katika ghasia hizo.

Baraza kuu la kijeshi-SCAF- ndio linalosimamia utaratibu wa kurejesha utawala kwa raia.
Licha ya ahadi za kuachia madaraka na kuharakisha utaratibu huo , baadhi ya waandamanaji wanahofu kuwa huenda viongozi hao wa kijeshi wananuia kung'ang'ania madaraka. Waandamanaji wanataka utawala wa kijeshi kuondoka kabla ya uchaguzi wa wabunge kufanywa.
Majeruhi katika maandamano Misri
Majeruhi katika maandamano Misri
Wakati huohuo raia wengi wa Misri wanataka uchaguzi uendelee kama ulivyopangwa. Kundi moja lenye ushawishi mkubwa nchini humo linalojulikana kama "Muslim Brotherhood" ambalo linatarajiwa kufanya vizuri katika uchaguzi, haliwaungi mkono waandamanaji katika medani ya Tahrir.

Wakati hayo yanaendelea maandamano ya kuunga mkono uchaguzi yanaandaliwa karibu na jengo la wizara ya mashauri ya ndani. 

Huko Washington, Ikulu ya White House imesema madaraka nchini Misriyanapaswa yahamishiwe kwa raia haraka iwezekanavyo.

Taarifa kutoka Ikulu ya White House ilisema "Marekani inaamini kuwa serikali mpya ya Misri inapaswa ipewe mamlaka kamili na thabit haraka iwezekanavyo."

Televisheni ya taifa ilisema kuwa jeshi limemteua aliyekuwa wakati mmoja Waziri Mkuu Kamal Ganzouri kuunda serikali mpya baada ya aliyemtangulia kujiuzulu.

Maelfu ya watu walikusanyika katika medani ya Tahrir kushiriki katika kile waandaaji wanasema ni Ijumaa ya mwisho ya fursa ya kutoa dukuduku lao la kutaka jeshi liachie utawala.

Shirika la AFP limesema kuwa Imamu aliyeongoza swala ya Ijumaa mjini Cairo alitoa wito kwa jeshi kuachia madaraka na kusema kuwa waandamanaji watasalia katika medani hiyo hadi matakwa yao yatakapotimizwa.

Waandamanaji wameushutumu uteuzi wa Bw. Ganzouri ambaye aliongoza serikali ya Misri kutoka mwaka 1996 hadi 1999 chini ya Hosni Mubarak.

No comments:

Post a Comment