Tangaza Biashara yako hapa

Friday, November 25, 2011

Chadema wang`aka mkutano wao na Kikwete kuingiliwa

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), wamepinga ushauri wa Kamati Kuu (CC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, kukutana na vyama vyote vya siasa badala ya Chadema peke yake.

Wa kwanza kupinga agizo la CC-CCM ni Chadema kupitia Kaimu Katibu Mkuu wake, Victor Kimesera.
Kimesera, ambaye ni Katibu Mtendaji Ofisi ya Katibu Mkuu wa Chadema, alisema jana jijini Dar es Salaam kuwa wanaopaswa kukutana na Rais Kikwete ni Chadema peke yake.
Hivyo, akasema Chadema hawako tayari kukubali kushirikiana na chama kingine chochote katika hilo kwa sasa.
“Sisi (Chadema) ndio tulioomba kukutana na Rais Kikwete. Hatukuwaombea wengine. Wao (vyama vingine) kama wana haja ya kukutana na Rais Kikwete waombe siku yao,” alisema Kimesera.
Alisema Chadema ilimuomba Rais Kikwete kukutana naye kwa ajili ya kujadili juu ya mchakato wa kupata kKatiba mpya na hawakuiomba CC-CCM suala hilo.
Kutokana na hilo, alisema wanamuachia Rais Kikwete na vyama vingine vya siasa kuamua lini wakutane. “Maamuzi yafanywe na wahusika, siyo na Kamati Kuu (ya CCM),” alisema Kimesera.
KAFULILA NAYE APINGA
Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, amesema haoni mantiki ya agizo hilo la CC-CCM.
“Uamuzi wa kwamba, tukutane vyama vyote na Rais sioni mantiki yake badala yake Rais akutane na wanaotaka kukutana naye,” alisema Kafulila.
Aliongeza: “Binafsi sioni sababu na sitegemei lolote kutoka kikao cha namna hiyo na Rais. Sisi hatukutoka bungeni ili tukutane na Rais baadaye.”
Alisema wanaamini CCM, serikali na hata Rais Kikwete mwenyewe hawana dhamira ya kweli katika ajenda ya katiba tangu mwanzo.
“Na hawatakuwa na dhamira hiyo hata baadaye kwa kuwa katiba wanayotaka wananchi ni msumari kwa chama na serikali ya CCM,” alisema Kafulila, ambaye pia ni Katibu Mwenezi wa NCCR-Mageuzi Taifa.
Alisema ushahidi unaothibitisha kuwa serikali haiko tayari kwa jambo hilo upo wazi.
Kafulila alisema ushahidi wa kwanza umethibitika katika msimamo wa CCM wa tangu mwanzo kwa kukataa kuweka ajenda ya katiba mpya kwenye Ilani yake ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana, licha ya msukumo wa umma kuhusu suala hilo kuwa mkubwa.
Alisema wa pili, umethibitishwa na Mwansheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, na Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani, ambao kabla ya tamko la Rais Kikwete kuridhia mchakato huo, kwa nyakati tofauti walikaririwa wakisema kwamba jambo hilo halina umuhimu wowote kwa sasa na kwamba, hadi leo bado hawajafuta kauli zao.
Ushahidi wa tatu, alisema Aprili, mwaka huu Baraza la Mawaziri, ambalo Mwenyekiti wake ni Rais, lilipitisha muswada mbovu wa sheria ya mabadiliko ya katiba kuliko miswada yote kiasi cha kuamsha hasira za umma, ambao walidiriki kuuchana hadharani na kutaka urejeshwe serikalini.
Alisema ushahidi wa nne umethibitika muswada huo uliporejeshwa serikalini na baadaye kuletwa mpya, ambapo bado serikali na CCM walishinikiza Bunge lijadili na kupitisha kabla ya umma kupata nafasi ya kujadili kama ilivyotakiwa kwa mujibu wa kanuni.
Jumatatu Chadema kilitangaza kuwa kinataka kukutana na Rais Kikwete kuzungumzia suala la katiba, baada ya wabunge wake kususia mjadala wa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya mwaka 2011.
Jumanne, Rais Kikwete aliwajibu kwa kuwakubalia na kuagiza kuwa maandalizi ya mkutano huo yaanze.
Katika kutekeleza azma hiyo ya kuonana na Rais, Chadema iliunda timu ya watu saba chini ya Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe, ambayo imepewa kazi ya kushughulikia suala hilo.
Wengine ni Katibu Mkuu, Dk. Slaa; Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Said Arfi; Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Issa Mohamed; wajumbe wa Kamati Kuu, Profesa Mwesiga Baregu na Profesa Abdallah Safari pamoja na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Hata hivyo, CC ya CCM juzi ilimshauri Rais Kikwete kukutana na vyama vyote vyenye wabunge kwa ajili ya kupanua wigo wa mawazo kuhusu katiba mpya.
Katibu wa Unezi na Itikadi wa CCM, Nape Nnauye, alisema CCM inaamini kuwa njia ya majadiliano waliyoitumia Chadema katika kutafuta haki ni nzuri na fursa hiyo ikitumiwa vizuri, inaweza kuleta maelewano mazuri na faida kwa jamii.

ASKOFU: WABUNGE HAWAJUI KINACHOENDELEA KATIKA MCHAKATO
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Iringa, Dk. Owdenberg Mdegella, amesema utata unaojitokeza hivi sasa wa wananchi kuonyesha nia ya kuupinga wazi wazi muswada huo, unatokana na baadhi ya watu, wakiwamo wabunge, kutojua kinachoendelea katika mchakato huo.
Alisema wapo wajanja wachache wanaojua kitakachotokea baadaye katika mchakato huo, lakini wengi wao hawajui kinachoendelea na kwamba, wamo katika kundi linalobebwa katika mchakato huo.
Askofu Mdegella alisema hayo jana wakati akihojiwa na Kituo cha Redio Furaha. “Swali kubwa katika marekebisho ya katiba duniani kote ni hili. Nani anachukua usukani wa kuhakikisha anajua kila sentensi, kila koma pamoja na nukta. Huwa serikali inatumia uzembe wetu wa kutokusoma kuingiza baadhi ya mambo, ambayo hayakuwamo. Hii ni hatari kubwa kama hatutakuwa makini,” alionya Askofu huyo.
Aliilaumu Chadema kwa kususia kushiriki mjadala wa muswada huo bungeni, akidai kwamba, kitendo hicho hakikuwa sahihi kwa kuwa kiliwaruhusu wabunge wa CCM kuupitisha kirahisi.
“Mimi nafikiri kitendo kile cha Chadema kutoka bungeni kwa ajili ya kususia muswada wa sheria ya marejeo ya katiba, hakikuwa sahihi kwa sababu kiliwaruhusu wabunge wa CCM kuupitisha muswada huo kirahisi…Kama wangekuwa ndani, nafikiri CCM wasingeupitisha kirahisi namna hiyo na hapo ndipo hoja yao ingeonekana ina nguvu,” alisema.
Kuhusu madaraka ya Rais, Askofu huyo alisema ni vyema yakapimwa upya na kushauri kuwa katika katiba mpya ijayo, Rais asipewe madaraka makubwa, badala yake apewe madaraka yanayoweza kuhojiwa kikatiba.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment