TANZANIA inahitajika kuwa na sera kwa ajili ya kusimamia viwanda vinavyozalisha nguo na ambavyo vinatumia pamba inayolimwa hapa nchini, ili kuleta ushindani kwa bidhaa zinazoingizwa kutoka China ambazo zimekuwa zikiingizwa nchini kwa kiasi kikubwa.
Mkurugenzi wa Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu Mzumbe iliyopo jijini Dar es Salaam, Profesa Andrew Mbwambo alisema hayo wakati akibadilishana mawazo na wasomi wenzake, viongozi wa serikali na watu wenye uzoefu katika uzalishaji katika sekta ya nguo ili kuweza kukamilisha utafiti anaoufanya na ambao unafanywa na wataalamu wa nchi saba za Afrika Mashairiki na Kusini mwa Afrika.
“Utafiti huu upo katika hatua ya awali kukamilika na unafanywa na nchi za Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika ambao unatarajia kuona ni jinsi gani nchi hizi zinajiadaa kuikabili nchi ya China inayokuja kwa kasi sana katika bidhaa za nguo ambazo zipo katika kila kona ya nchi hizi Tanzania ikiwa mojawapo,” alisema Profesa Mbwambo.
Alisema nchi zinazofanya utafiti huo ni pamoja na Kenya, Afrika Kusini, Ethopia, Lethoto, Madascar, Swaziland na Tanzania na lengo siyo kuwa kama China bali kuwa na mikakati ya kujiandaa ili kukabili na kusaidia kukuza uchumi na kuongeza ajira.
Alisema katika utafiti wake huo kwa upande wa Tanzania anatafuta kujua kwa nini viwanda hivyo baada ya kubinafsishwa vinakufa na vingine vimebaki kama vilivyo ili kufahamu tatizo na baadaye kuweza kuishauri serikali hatua za kuchukuliwa.
“Sasa hivi tunaendelea na utafiti, tumeona tuwashirikishe wazalishaji wenyewe kutoka viwandani, watunga sera na wasomi na baada ya kupata sababu ya kuelewa kuhusu tatizo hili tutaandika mapendekezo ya sera ili tuweze kuwa na sera nzuri katika eneo hili,” alisema Profesa Mbwambo.
Alisema nchi ikiwa na sera nzuri ya eneo hili la viwanda vya kuzalisha nguo itatoa fursa ya kutonyanyaswa na bidhaa za kutoka China na hiyo itatoa fursa tena kwa wakulima wa Pamba kupata soko la uhakika na nchi kufaidika zaidi.
Profesa Mbwambo alisema nchi ikiwa na viwanda vingi na kuweza kuuza nguo nzuri za Pamba, mablanketi mazuri na viatu kama inavyofanya kampuni ya Sun Flag Textile ya Arusha ambayo inauza nguo Marekani, Ulaya, India na Afrika ya kati na Mashariki taifa litapiga hatua kwa kasi kubwa kimaendeleo.
Alisema kukiwepo na Sera maalumu ya kuongoza viwanda vya nguo kama ilivyo kuwa huko nyuma nchi iliweza kuwa na viwanda vingi kwa kuwa baada ya kubinafsisha viwanda wawekezaji hao wengine waliamua kuuza kama chuma chakavu sasa lazima kuwe na sera ya kuongoza eneo hilo.
“Wataalamu wanasema kunatofauti ya soko huru na soko huria, soko huru hata ukienda Marekani kuna taratibu ambazo zinatakiwa kufuatwa kwamba lazima iwe na ubora na ukikosea moja huwezi kufanya biashara lakini soko huria ni kuingiza kila takataka”alisema Profesa Mbwambo.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Ukanda wa Uwekezaji (EPZA), Dk Adelhelm Meru akifungua washa hiyo alisema anashukuru utafiti huo ambao unaendelea kufanyika kwa kuibua masuala muhimu ambayo yatakuwa ni msaada wa nchi kuweza kuwa na sera nzuri katika eneo la sekta ya viwanda vya nguo ili kukabili bidhaa za nguo zinazotoka nje ya nchi.
“Utafiti huu unahusisha watalaamu mbalimbali kutoka Chuo Kikuu Mzumbe, Chuo Kikuu cha Nairobi na Vyuo vingine vya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika kwa lengo la kuona maendeleo ya zao la Pamba na sekta nzima ya viwanda vya nguo kuona tunajifunza nini ukizingatia China inapiga kasi kubwa na bidhaa zao zimetapakaa katika nchi hizi,” alisema Dk Meru.
Alisema ukweli ni kwamba huko nyuma Tanzania ilikuwa ikifanya vizuri sana kulikuwa na viwanda vya Mutex, Mwatex, Urafiki na Sunguratex lakini kwa kufikia miaka ya 1990 vilikufa kutokana na uchumi wa dunia kutetereka.
Alisema kwa sasa Serikali inafanya juhudi za makusudi kuhakikisha inafanya vizuri na uzoefu unaonyesha kuwa sekta ya viwanda ndiyo muhimu sana kwa uchumi wa nchi na utoaji wa ajira kwa wananchi.
Alisema Tanzania ni nchi inayozalisha Pamba kwa wingi laikini kwa bahati mbaya inauzwa nje ya nchi ikiwa ghafi ndiyo maana Serikali inahamasisha uwekezaji ili pamba hiyo iweze kutumika katika viwanda vya hapa nchini badala ya kuuzwa ikiwa ghafi.
No comments:
Post a Comment