Tatizo la kukosa choo watoto wadogo au kuwa na choo kigumu na jinsi ya kulitatua
Watoto wadogo hasa wale ambao bado wananyonya na ndio kwanza wamenzishwa vyakula vinginevyo zaidi ya maziwa, mara nyingi hupatwa na choo kigumu au kukosa choo kabisa hali tunayoiita kimombo, constipation.
Hali hiyo huanza pale mtoto anapoachishwa maziwa ya mama na kuanza kunyweshwa maziwa ya kopo au mengineyo au pia anapoanzishwa kula vyakula vingine zaidi ya maziwa. Mara nyingi watoto wanaonyonya maziwa ya mama huwa hawasumbuliwa na tatizo hilo, bali tatizo hilo huanza kujitokeza pale wanapoanza kulishwa vyakula vingine zaidi ya maziwa ya mama. Pia mama ambaye tayari mwenyewe anasumbuliwa na tatizo la kukosa choo, huenda mwanae pia akasumbuliwa na tatizo hilo.
Mtoto mwenye tatizo la kukosa choo huwa anapata choo wa shida huku akisumbuliwa na tumbo na kupata choo kigumu. Wakati mwingine hulia wakati akipata choo huku akijiminya na kukunja uso. Muone daktari iwapo mtoto ana umri wa chini ya mwezi mmoja na hajapata choo kwa siku 4.
Iwapo mtoto wako mchanga au mdogo ana tatizo la kukosa choo au kupata choo kigumu kwanza wasiliana na daktari au mpeleke hospitalini ili upate ushari wa daktari. Pia unashauriwa kujaribu njia zifuatazo:
1. Jaribu kumpa mtoto wako maji safi na salama kuanzia mililita 60 hadi 120 kwa siku. Punguza au ongeza kiasi hicho kwa kuzingatia jinsi hali ya mwanao inavyokuwa. Ni bora maji ya mtoto yachemshwe na kufunikwa vyema.
2. Iwapo maji hayasaidii, jaribu pia kumpa juisi za matunda. Mpe mtoto wako juisi ya tufaha (apple), pea au prune iliyotengenezwa kwa kutumia maji salama na safi kila siku. Anza kwa mililita 60 hadi 120 kwa siku na punguza au ongeza kiasi hicho kwa kuzingatia jinsi hali ya mwanao inavyokuwa.
3. Jitahidi kumpa mwanao chakula chenye ufumwele au fiber. Iwapo mwanao ameanza kula vyakula vigumu, basi mpe vyakula vyenye ufumwele kuliko vyakula vyenye wanga, kama vile tumia unga wa shayiri au tunda la apple na pea lililopondwa pondwa vyema na kuwa kama uji. Epuka kumpa mtoto cereal ya mchele au uji wa mchele kama anatatizo la kukosa choo au kufunga choo.
4. Jiepushe kumpa mtoto wako vyakula vyenye wanga na sukari na vyakula vinavyotengenezwa kwa unga uliokobolewa.
5. Mpake mwanao mafuta kidogo sehemu inayotoka choo kikubwa ili kurahisisha utokaji wa kinyesi. Usitumia mafuta ya madini (mineral oil) au dawa za kulainisha choo na za kuharishwa katika kutibu tatizo hilo la kukosa choo la mtoto.
6. Kukosa choo watoto wadogo mara chache huwa kunasababishwa na magonjwa kama vile Hirschsprung ugonjwa wa kumee neva katika utumbo, au Cystic Fibrosis. Muone daktari au mpeleke mtoto wako hospitalini kama tatizo hilo la kukosa choo linaendelea hata baada ya kubadilisha aina ya chakula cha mtoto au linaambatana na dalili nyingine kama vile kutapika au mtoto kukosa utulivu na kuhangaika.
7. Kuna baadhi ya watoto wanakosa choo au kuwa na choo kigumu kutokana na kutumia maziwa ya ng’ombe. Iwapo umetumia dawa na umefuata maelekezo ya kuondoa ukosefu wa choo na hukufanikiwa. Katisha kumpa mtoto maziwa ya ng’ombe kwa siku mbili au tatu, baada ya siku hizo iwapo bado hajaacha choo badi endelea kumpa maziwa hayo, na pengine tatizo hilo halisababishwi na maziwa ya ng’ombe.
8. Mwogeshe au mweke mwanao katika beseni la maji ya uvuguvugu na hakikisha maji yanafika hadi kifuani. Mkande mtoto tumbo lake wakati akiwa majini na njia hiyo husaidia kulegeza misuli ya mwili wa mtoto, na kumsaidia kupata chook wa urahisi.
N.B Ukosefu wa choo kwa watu wazima baadhi ya wakati huandamana na magonjwa kama vile Arthritis, Appendicitis, Cataract, saratani, shinikizo la damu, Rheumatism na kadhalika lakini kwa watoto huenda tatizo hilo likawa halisababishwi na maradhi hayo.
Utafiti unaonyesha kuwa hakuna uhusiano wowote kuhusu kukosa choo mtoto na kupewa nyongeza ya chuma au Iron Supplement. Hivyo usimkatishe kumpa mwanao chuma iwapo anakosa choo. Kwani chum ni muhimu sana katika kuzuia upungufu wa damu mwilini kwa mtoto wako mdogo.
No comments:
Post a Comment