Tangaza Biashara yako hapa

Friday, November 25, 2011

Maghembe ahimiza zana bora kilimo cha tumbaku


Serikali imewaasa wakulima wa tumbaku duniani kupuuza vitisho na upinzani dhidi ya zao hilo na badala yake walime zao hilo kwa wingi zaidi huku wakifuata kanuni na taratibu za ulimaji wa zao hilo kama zilivyowekwa na serikali zao.

Kauli hiyo ilitolewa mjini hapa juzi na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Jumanne Maghembe, wakati akifungua Mkutano wa Asasi ya Kimataifa ya Wakulima wa Tumbaku(ITGA).

Aidha, Waziri Mghembe amewataka wadau wa tumbaku katika nchi zinazoendelea kuchagiza mabadiliko ya wakulima wao ili wafikie viwango vya wale wa nchi tajiri duniani, ikiwemo kuachana na zana za kilimo duni kama vile jembe la mkono ambalo hudumaza kipato cha wakulima.

"Wakati umefika sasa kwa wakulima wetu kubadilika na ili wawafikie wenzao wa nchi tajiri kwa kutumia mikopo ili kubadilisha zana za kilimo, na badala yake watumie jembe la ng’ombe na matrekta. Tutakapofikia hapo huu wastani wa 0.8 hadi hekta moja kwa mkulima tutaachana nao,” alisema katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mohammed Muya.

Profesa Maghembe aliishauri sekta ya tumbaku kuchukua hatua dhidi ya upotevu wa zao hilo wakati wa mavuno, ambapo kwa sasa wakulima hupoteza hadi asilimia 35, huku akisisitiza umuhimu wa sekta kujikita katika uhamasishaji wa ujenzi wa mabanda kukaushia, kufungia na yale ya kuhifadhia zao hilo.

Profesa Maghembe alisema sekta ya tumbaku ndiyo pekee nchini yenye sera maalum utunzaji mazingira kwa upandaji miti, akitoa mfano kwamba tangu msimu wa mwaka 2009/2010 miti zaidi ya milioni 20 imekuwa ikipandwa na wakulima wa zao hilo kila mwaka nchini.

Alizitaja faida za zao hilo ikilinganishwa na mazao mengine mbadala kama vile bei kubwa na imara wakati wote pamoja na soko la uhakika hivyo huchangia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha na uchumi wa watu vijijini.

Msemaji kutoka kampuni ya Universal Leaf ya Marekani ambayo ni kampuni mama ya Kampuni ya Tumbaku Tanzania (TLTC), Barbara Martelini, alisema wakati umefika kwa sekta hiyo kuelimisha umma namna mambo yanavyokwenda katika sekta hiyo ili kupunguza upotoshaji uliopo.

Msemaji mwingine kutoka Kampuni ya British American Tobacco (BAT), alisema kampuni yake iko makini kutunza biyoanuai miongoni mwa wakulima wa tumbaku ambayo hufanya kazi nao, na inao mkakati maalum wa kuwalemisha wakulima hao waendelee kufanya hivyo wakati wote.

Naye Mkurugenzi mkuu wa Bodi ya Tumbaku nchini (TTB), Frank Urio, alisema tumbaku ni zao muhimu kwa maendeleo ya uchumi wan chi kwani mpaka sasa imeajiri zaidi ya familia 130,000 nchini ambao wamejiunga katika vyama saba vya ushirika wa kilimo.
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment