Tangaza Biashara yako hapa

Sunday, November 20, 2011

Kuna uhuru wa vyombo vya habari katika nchi huru kama Tanzania?




  • Japo Tanzania ni nchi yenye uhuru mkubwa wa habari, mimi nadhani uhuru huu hautumiwi vizuri na ubora wa habari tunazoshindiliwa kila siku hauridhishi. Kwa mfano, ni magazeti machache sana yanayoandika habari za kweli na zilizofanyiwa uchunguzi wa kina, habari zilizojaa ushahidi, data na hoja hakikifu yakinifu. 
  • Magazeti mengi - hata yale yanayojidai kuwa ni dhati pevu - yamejikita katika kuandika habari zilizofanyiwa uchambuzi nusunusu, habari ambazo japo kwa juu zinaonekana kama za kweli, ukisoma kwa uangalifu utakuta kwamba ama lojiki na hata data zilizotumiwa katika kufanyia majumuisho ya habari hizo hazikubaliki. Matokeo yake habari nyingi zinaandikwa kwa kuripuliwa na zinaonekana kuwa kama za udakudaku tu; na zilizojaa mihemko inayotokana na ushabiki wa kisiasa uliokithiri.
  • Kwa vile udaku ndiyo unaopendwa sana na wasomaji, inawezekana pengine magazeti mengi yanafanya hivi ili yaweze kuvutia wasomaji. Mkanganyiko unazidi zaidi kwa sababu wanajamii wengi bado wanaamini kwamba kila kinachotiwa katika maandishi, kusikika kwenye redio au runinga basi ni lazima kiwe cha ukweli. 
  • Matokeo yake tunakuwa na jamii inayoshabikia mambo bila kuyaelewa sawasawa, jamii iliyojikita katika kuamini udaku na inayoweza kuyumbishwa kirahisi. Ndiyo maana ni rahisi sana kumchafulia mtu jina kama ukitaka. Kama una "bifu" na Matondo na akatokea kuwa na nafasi kubwa katika jamii, basi jidamke na kusema kuwa Matondo ni fisadi na akaunti yake aliyoficha Marekani ina mamilioni ya dola. Na kesho yake utakuta habari hii imetapakaa katika kurasa za mbele za magazeti  - hata yale yanayojidai kuwa makini. 

  • Hakuna gazeti ambalo litakaa chini na kujaribu kutafuta ukweli na kuthibitisha chanzo na uhalali wa habari kama hii. Na kwa vile jamii nayo bado inaamini (na hata kutegemea) kwamba kila kitu kinachoandikwa katika magazeti ni cha ukweli basi kuanzia siku hiyo mlengwa wa habari hizi atajulikana kama fisadi, gamba n.k. Na kama hana ujasiri wa kusimama na kujitetea kama alivyofanya Sumaye hapa chini basi jamii daima itamtazama kwa jicho la hatihati. 
  •  

  • Lengo langu hapa siyo kuwatetea mafisadi na nadhani msimamo wangu kuhusu UFISADI na mambo mengine katika jamii unaeleweka kwa wasomaji wa blogu hii. Ninachokisema hapa ni kwamba, kama jamii ni lazima tuwe makini na habari nusunusu tunazolishwa na vyombo vyetu hivi vya habari. Na litakuwa jambo jema kama tutaweza kuzitambua habari za kidaku kama wenzetu hawa na kuzipa uzito wake unaostahili.   

  • Waandishi wa habari, mnalo jukumu kubwa sana katika ukombozi wa jamii yetu na kabisa msijaribu kuliteteresha jukumu hili zito. Kama tulivyoona katika uchaguzi mkuu uliopita, mabadiliko mema yanatokea  katika nchi yetu na nyakati zinabadilika. Isaidieni jamii katika juhudi za kujitafuta kwake. Shirikini vyema katika kuhakikisha kwamba tunakuwa na jamii makinifu na yenye uwezo wa kuhoji ukweli wa mambo na siyo kushabikia udaku kiholela - jamii ambayo ikidanganywa au kupewa habari au ahadi za kidaku, basi iwe na uwezo wa kusimama na kusema hapa mmetudanganya; na mkiendelea kutudanganya basi tutawanyang'anya madaraka tuliyowapa!

No comments:

Post a Comment